ZANZIBAR-Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema ahadi ya kupatikana katiba mpya Tanzania iko pale pale kwakuwa ni ahadi ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kabla hajaondoka madarakani mwaka 2030.
Aidha, CCM kimeupongeza msimamo uliotolewa na Makamu wa Rais Dkt Emmanuel Nchimbi kusisitiza azma kuandikwa katiba hiyo.
Kauli hiyo imetamkwa nanLatibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis aliyesisitiza katiba mpya ni ahadi ya CCM kwa Watanzania.
Mbeto alisema Rais Dk Samia alitoa ahadi hiyo katika mkutano wa uzinduzi kampeni za Uchaguzi Mkuu za ccm zilizofanyika viwanja vya Tanganyika Packers jijini Dar es Salaam.
Alisema kauli ya Dk Nchimbi ni msisitizo wa dhati kufuatia maamauzi ya ccm na serikali zake ,hivyo matamshi yake yanakwenda sambamba na ahadi ya Rais Dk Samia.
"Kwa dhati kabisa nipende kumpongeza Makamu wa Rais Dk Nchimbi kuwakumbusha Watanzania ahadi ya Katiba mpya. CCM na Kama vilivyoruhusiwa vyama vingi katiba itapatikana,"amesema Mbeto.
Aidha, Katibu huyo Mwenezi, aliwataka watanzania kuendelea kuiamini CCM kwakuwa ni chama kinachopitisha maamuzi magumu bila jazba,pupa au kwa shinikizo .
"Maamuzi yoyote yanayobeba maslahi ya Umma hayafanyiki kwa kiherehere.Lazima kufanyike tathmini za kina ,uchambuzi wa kutosha huku mkizipitia faida na hasara za maamuzi husika."
Katibu Mwenezi huyo,alisema inapotamkwa kauli ya Rais, Makamu wa Rais au Waziri mkuu, kauli hiyo hutokana na utatu wa kimaamumuzi ya chama, serikali kwa mujibu wa vikao.
"Katiba iliopo ya Tanzania ya mwaka 1977 ni katiba bora sana.Ingekuwa si katiba bora Taifa lisingefikisha miaka zaidi ya sitini.Ni uamuzi wa watanzania wenye kupata katiba nyingine au la,"alisisitiza.
Mbeto aliendelea kufafanua kuwa jukumu la kupatikana katiba halihitaji kikiri zinazoweza kuhatarisha Amani na Utulivu, badala yake ni mambo ya kujadiliana kwa njia za kiungwana.
Akielezea kwa undani, Mwenezi huyo alisema jukumu la kuandikwa kwa katiba mpya si la Mashirika hiari ya kijamii, watetezi wa Haki za binadamu,upinzani au nchi washirika bali ni la watanzania wenyewe.
"Ahadi na hatma kupatikana katiba mpya iko mikononi mwa watanzania wenyewe.Dhamana ya serikali za CCM ni kuandaa mazingira bora na wezeshi ili kupata katiba inayokidhi haja na matakwa ya nyakati,"alifafanua.
