ARUSHA-Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Uwanja wa Arusha unaojengwa jijini Arusha kwa ajili ya kutumika katika fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Akiwa katika ziara hiyo, Dkt. Nchimbi amepongeza maendeleo ya ujenzi wa uwanja huo na kueleza kuwa ni faraja kuona ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuwezesha Tanzania kuwa mwenyeji wa michuano hiyo ikitekelezwa kikamilifu kupitia miradi mbalimbali ya miundombinu ya michezo.
Makamu wa Rais amemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kutoa fedha zinazowezesha ujenzi wa uwanja huo kuendelea kwa kasi na kuhakikisha unakamilika kwa wakati ili kuifikia azma ya nchi ya kuwa mwenyeji wa AFCON 2027.
Aidha, Dkt. Nchimbi ameipongeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, wakandarasi pamoja na mshauri elekezi kwa kazi kubwa wanayoifanya katika utekelezaji wa mradi huo muhimu wa kimkakati.
Vilevile, Makamu wa Rais amewataka viongozi wa Wizara pamoja na Mkoa wa Arusha kusimamia kwa karibu agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha barabara zote zinazotumika kufika katika uwanja huo zinakamilika kwa wakati, ili kuwezesha miundombinu yote muhimu kuwa tayari kabla ya kuanza kwa michuano ya AFCON 2027.








