NA DIRAMAKINI
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Balozi Dkt.Emmanuel Nchimbi amewataka Watanzania kuendelea kudai kupatikana kwa Katiba mpya yenye maridhiano ya kitaifa, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha haki za binadamu, utawala bora na demokrasia nchini.
Dkt.Nchimbi ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam leo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 15 wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), akisisitiza kuwa Katiba ni msingi muhimu wa kuweka mfumo wa utawala unaozingatia haki, wajibu na maslahi ya wananchi wote.Akizungumza katika mkutano huo, Makamu wa Rais amesema endapo angepewa nafasi ya kuwaambia Watanzania jambo moja pekee, angewasihi kuendelea kupambania upatikanaji wa Katiba mpya yenye makubaliano mapana ya kitaifa.
“Pambaneni mpate Katiba ambayo ina makubaliano ya wadau wote, Katiba yenye muafaka katika taifa, Katiba itakayotupeleka mbele miaka 50 inayokuja na ambayo kila Mtanzania atajivunia kwa sababu inajali maisha ya mtu na kuheshimu haki za raia wake,”amesema.
Amesisitiza kuwa,Katiba mpya inapaswa kuwa matokeo ya mchakato shirikishi unaowahusisha wadau mbalimbali, ili kuhakikisha inakuwa na uhalali, uaminifu na kukubalika kwa wananchi kwa upana.
Kwa mujibu wa Dkt.Nchimbi, Katiba yenye maridhiano ya kitaifa inaweza kuwa nyenzo muhimu ya kuimarisha misingi ya demokrasia, uwajibikaji wa viongozi, ulinzi wa haki za binadamu na utawala unaozingatia sheria.
Amesema,haki za binadamu si suala linalohusu sheria pekee, bali ni jambo linalogusa maisha ya kila siku ya kila Mtanzania, ikiwemo namna wananchi wanavyopata huduma, wanavyoshiriki katika uongozi na wanavyolindwa dhidi ya vitendo vya ukiukwaji wa haki.
Kauli hiyo inatolewa wakati mjadala kuhusu upatikanaji wa Katiba mpya ukiendelea nchini. Mchakato wa kuandika Katiba mpya ulianza mwaka 2011 chini ya Serikali ya Rais wa Awamu ya Nne, Dkt.Jakaya Kikwete, lakini ulikwama mwaka 2014 kabla ya kufikia hatua ya kupigiwa kura ya maoni.
Hata hivyo, Serikali imeendelea kuonesha dhamira ya kuufufua mchakato huo. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewahi kueleza kuwa mchakato wa Katiba mpya unatarajiwa kuendelea kabla ya mwaka 2030, huku Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 pia ikiahidi kuendeleza mchakato huo.
Akizungumza mbele ya wadau hao wa haki za binadamu, Dkt.Nchimbi amesisitiza umuhimu wa kujenga Tanzania inayoheshimu utu, haki na uhuru wa wananchi, akisema jukumu la kulinda na kuendeleza misingi hiyo linahitaji ushirikiano wa Serikali, taasisi za haki za binadamu, asasi za kiraia na wananchi kwa ujumla.
Amesema,mjadala wa Katiba mpya unapaswa kuendeshwa kwa utulivu, kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa na kwa kujenga maridhiano badala ya migawanyiko.
Mkutano Mkuu wa THRDC unawakutanisha wadau wa haki za binadamu kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kujadili hali ya haki za binadamu, changamoto zinazolikabili Taifa pamoja na mikakati ya kuimarisha ulinzi na utekelezaji wa haki za msingi za wananchi.
Mkutano huo pia unatarajiwa kutoa fursa kwa wadau kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha utawala bora, demokrasia na uwajibikaji katika uongozi wa umma.