NA GODFREY NNKO
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema, kutiwa saini kwa Tamko la Pamoja la Maridhiano kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ACT Wazalendo ni hatua ya kihistoria inayofungua ukurasa mpya wa kuimarisha umoja wa kitaifa, utulivu wa kisiasa na maendeleo endelevu ya Zanzibar.
Dkt.Mwinyi ametoa kauli hiyo Julai 9, 2026, katika hafla ya utiaji saini wa tamko hilo iliyofanyika Ikulu Zanzibar na kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan,viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini,mabalozi wa nchi mbalimbali, viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na wageni mbalimbali.Amesema, tamko hilo linaweka msingi imara wa kuendeleza maridhiano ya kisiasa na kuimarisha mshikamano wa wananchi wa Zanzibar, hatua ambayo itaongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa manufaa ya wananchi wote.
"Hatua hii ya leo ni muhimu sana kwa wananchi wa Zanzibar na Watanzania kwa ujumla katika kuimarisha mshikamano, maridhiano ya kitaifa na kufanikisha jitihada zetu za maendeleo,"amesema Dkt. Mwinyi.
Maridhiano yawe chachu ya maendeleo
Rais Mwinyi ameeleza kuwa,mafanikio ya maridhiano hayo yataongeza imani ya wananchi, wawekezaji, wafanyabiashara na washirika wa maendeleo, jambo litakalochochea uwekezaji zaidi na kukuza uchumi wa Zanzibar.
Amesema,mazingira ya amani, utulivu na mshikamano ni nguzo muhimu katika kuvutia mitaji, kuongeza shughuli za kiuchumi na kuimarisha ustawi wa wananchi.
"Ninaamini mwafaka tunaoukusudia utaongeza imani kwa wananchi na wadau mbalimbali, wakiwemo wawekezaji na washirika wa maendeleo, katika kuendelea kushirikiana na Zanzibar kutekeleza mipango yetu ya maendeleo," amesema.
Aidha, ameeleza kuwa,maridhiano hayo yanafungua njia ya utekelezaji wa matakwa ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kuhusu kuimarisha umoja wa kitaifa, huku akiahidi kusimamia kwa uwazi na uadilifu awamu ya pili ya mazungumzo kati ya pande husika.
Kwa mujibu wa Dkt.Mwinyi, hatua inayofuata itakuwa kufanya majadiliano ya kina kuhusu ajenda zilizokubaliwa ili kuhakikisha maslahi ya Zanzibar yanawekwa mbele wakati wote katika kujenga mustakabali bora wa visiwa hivyo.
Awapongeza waliosimamia mazungumzo
Katika hotuba yake, Dkt.Mwinyi amewashukuru wajumbe wa kamati iliyosimamia awamu ya kwanza ya mazungumzo kwa kuweka mbele maslahi ya Zanzibar badala ya maslahi binafsi au ya kisiasa.
Pia amewapongeza Marais Wastaafu wa Zanzibar, Dkt. Amani Abeid Karume na Dkt.Ali Mohamed Shein, pamoja na viongozi wa ACT Wazalendo akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho, Othman Masoud Othman na Makamu Mwenyekiti, Juma Duni Haji, kwa mchango wao katika kufanikisha hatua hiyo muhimu.
Amebainisha kuwa,Zanzibar ina historia ya mafanikio katika maridhiano ya kisiasa, akirejea mchakato uliowezesha kufanyika kwa marekebisho ya Katiba na kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, akisema uzoefu huo unatoa matumaini makubwa kwamba safari ya sasa nayo itafikia mafanikio yaliyokusudiwa.
Rais amewataka viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini, asasi za kiraia na wananchi kwa ujumla kuunga mkono mchakato huo kwa dhati, akisisitiza kuwa maendeleo ya Zanzibar yanategemea mshikamano, amani na ushirikiano wa wananchi wake.
Othman:Maridhiano ni kwa manufaa ya Wazanzibari wote
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman amesema kutiwa saini kwa makubaliano hayo ni hatua muhimu ya kujenga Zanzibar yenye umoja, utulivu wa kisiasa na maendeleo ya kudumu, akisisitiza kuwa mchakato huo haukusudii kunufaisha vyama vya siasa pekee bali wananchi wote.
Amesesema mazungumzo yaliyoanza Novemba 9, 2021, yameweka msingi wa kutafuta suluhisho la kudumu kwa changamoto za kisiasa zilizojitokeza baada ya uchaguzi.
"Nchi nyingi zilizopiga hatua ya maendeleo zimejenga kwanza mshikamano wa kijamii, utawala wa sheria, uwajibikaji, utulivu wa kisiasa na amani endelevu. Haya ndiyo tunayotafuta kwa Zanzibar kupitia maridhiano haya,"amesema.
Amefafanua kuwa,hatua zinazofuata zitahusisha kuundwa kwa kamati ya pamoja itakayochambua maeneo yote yaliyokubaliwa na kupendekeza namna ya kuyafanyia kazi, huku tume ya utekelezaji itakayoundwa kwa mujibu wa sheria ikisimamia utekelezaji wa makubaliano hayo.
Mageuzi ya taasisi za umma yapewa kipaumbele
Othman amesema,maeneo yatakayopatiwa kipaumbele katika mchakato huo ni pamoja na kujenga imani na kuaminiana, kupitia upya Katiba, kuboresha mfumo wa uchaguzi, kuimarisha utumishi wa umma, mfumo wa utoaji haki pamoja na serikali za mitaa ili kuimarisha utawala bora na ufanisi wa taasisi za umma.
Amesisitiza kuwa,maridhiano hayo ni mkakati wa muda mrefu wa kujenga taasisi imara, mazingira bora ya uwekezaji na uchumi wenye ushindani ambao utaifanya Zanzibar kuwa kitovu cha biashara, huduma na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.
"Hatua hizi si kwa faida ya vyama vya siasa tu. Ni kwa manufaa mapana ya Zanzibar na vizazi vijavyo. Tunajenga taasisi imara, uchumi wenye ushindani na mfumo wa haki utakaoweka mazingira bora ya uwekezaji na maendeleo,"amesema.
Atoa wito wa kujenga imani
Mwenyekiti huyo wa ACT Wazalendo amesema, bado yapo makundi yenye mitazamo tofauti kuhusu mchakato wa maridhiano, ambapo baadhi wana matumaini makubwa, wengine wamekata tamaa kutokana na uzoefu wa makubaliano yaliyopita, huku kundi dogo likipinga kabisa juhudi hizo.
Amewataka viongozi wa kisiasa, viongozi wa dini na jamii kwa ujumla kushirikiana kujenga imani kwa wananchi ili kuhakikisha makubaliano hayo yanatekelezwa kwa uaminifu na kuleta matokeo yaliyokusudiwa.
"Hawa waliokata tamaa wana hoja kutokana na walikotoka, lakini wakiona dhamira ya kweli watakuwa sehemu ya mafanikio ya mchakato huu. Wanaopinga kabisa ni wachache, lakini hatupaswi kuwapa nafasi ya kuzuia mustakabali wa Zanzibar,"amesema.
Aidha, Othman amemshukuru Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuongoza mchakato huo kwa busara na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za maridhiano na kuhimiza viongozi kusikiliza hata yale ambayo hayasemwi wazi.
Amesema,mafanikio yaliyopatikana ni matokeo ya hekima, uvumilivu na uzalendo wa viongozi wa pande zote, akieleza kuwa maridhiano hayo yanaweka msingi wa kujenga Zanzibar yenye amani, mshikamano, utawala bora na maendeleo endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.