Mbwana Samatta astaafu kuichezea Taifa Stars baada ya miaka 15 ya historia na mafaniko

NA DIRAMAKINI

NAHODHA wa zamani wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Mbwana Ally Samatta ametangaza rasmi kustaafu kuitumikia timu hiyo baada ya kuitumikia kwa takribani miaka 15, akihitimisha safari iliyojaa mafanikio makubwa na kuweka rekodi mbalimbali katika historia ya soka la Tanzania.
Katika taarifa yake kwa umma, Samatta amesema amefikia uamuzi huo baada ya kutafakari kwa kina, akieleza kuwa amejivunia kuitumikia Tanzania kwa kipindi chote hicho na kwamba sasa umefika wakati wa kizazi kipya cha wachezaji kupewa nafasi ya kuendeleza mafanikio ya Taifa Stars.

"Baada ya kutafakari kwa kina, ninatangaza rasmi kustaafu kuitumikia Timu yangu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kuanzia leo. Ulikuwa wakati mzuri na wa kipekee katika maisha yangu kuwa mchezaji wa Timu ya Taifa kwa takribani miaka 15 na najisikia fahari kusema nashukuru kwa nafasi hii," amesema Samatta.

Mshambuliaji huyo amesema miaka 10 aliyohudumu kama nahodha wa Taifa Stars imeacha alama kubwa katika maisha yake ya soka, akieleza kuwa miongoni mwa mafanikio makubwa aliyoshiriki ni kuiongoza Tanzania kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mara tatu pamoja na kuweka historia ya kufuzu hatua ya 16 bora ya mashindano hayo kwa mara ya kwanza.

"Naamini huu ni wakati wa vipaji vipya kupewa nafasi ya kutufikisha kwenye hatua za juu zaidi," amesema.

Samatta ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa mchango wao katika kuifanya Taifa Stars kuwa ndoto ya kila mchezaji wa Kitanzania.

Aidha, ametoa shukrani kwa familia yake, wachezaji wenzake, marafiki, wadau wa soka na Watanzania wote kwa upendo na sapoti waliompa katika nyakati za mafanikio na changamoto.

Amesisitiza kuwa,licha ya kustaafu kuchezea Taifa Stars, ataendelea kulitumikia taifa kupitia maeneo mengine yanayohusiana na maendeleo ya soka kwa kutumia uzoefu alioupata katika maisha yake ya kimichezo.

"Nikijivunia Utanzania wangu, naahidi kuendelea kutoa mchango wangu kwa Timu ya Taifa katika maeneo mengine yaliyo ndani ya uwezo na uzoefu wangu," amesema.

Safari ya Samatta

Mbwana Ally Samatta aliyezaliwa Desemba 23, 1992, amebaki kuwa mmoja wa wachezaji wenye mafanikio makubwa zaidi kuwahi kutokea nchini Tanzania.

Ameandika historia kwa kuwa mchezaji wa kwanza wa Tanzania kucheza katika moja ya ligi tano bora barani Ulaya, hatua iliyofungua milango kwa wachezaji wengine wa Kitanzania kutafuta nafasi katika soka la kimataifa.

Umaarufu wake uliongezeka akiwa na klabu ya KRC Genk ya nchini Ubelgiji, ambapo aliisaidia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Ubelgiji (Jupiler Pro League) msimu wa 2018/19 huku akimaliza msimu huo akiwa miongoni mwa wafungaji bora wa ligi.

Katika maisha yake ya soka, Samatta amecheza zaidi ya mechi 400 za ushindani na kufunga mabao zaidi ya 150 katika ngazi ya klabu na timu ya taifa, mafanikio yaliyomweka miongoni mwa washambuliaji bora kabisa kuwahi kutokea Tanzania.

Kwa sasa anaitumikia klabu ya Le Havre AC inayoshiriki Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1), ambapo ameendelea kuonesha kiwango cha juu.

Mwezi Aprili 2026 alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi wa klabu hiyo baada ya kufunga mabao mawili muhimu katika mechi nne na kuisaidia timu kujinasua kutoka kwenye hatari ya kushuka daraja.

Aidha,kustaafu kwa Samatta kunahitimisha enzi ya mmoja wa viongozi na wachezaji walioandika historia kubwa katika soka la Tanzania, huku mchango wake ukitarajiwa kuendelea kuonekana kupitia maendeleo ya mchezo huo hata baada ya kuachana na majukumu ya kuchezea Taifa Stars.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here