Mheshimiwa Abdulla awataka wananchi kushirikiana na vyombo vya dola kudumisha amani na kuimarisha haki

NA DIRAMAKINI

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe.Hemed Suleiman Abdulla amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola katika mapambano dhidi ya uhalifu kwa kutoa taarifa zinazohusu vitendo vya uhalifu, kushiriki kutoa ushahidi pale inapohitajika na kuwa walinzi wa amani na utulivu unaoendelea kushuhudiwa nchini.
Mheshimiwa Abdulla ametoa wito huo leo katika Hoteli ya Madinat Al Bahr, Chukwani alipomwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwenye maadhimisho ya miaka 24 tangu kuanzishwa kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar.

Amesema,ushiriki wa wananchi katika kutoa taarifa na ushahidi ni nguzo muhimu katika kuhakikisha sheria zinatekelezwa kwa ufanisi na wahalifu wanawajibishwa kwa mujibu wa sheria, jambo linalochangia kudumisha amani, usalama na utawala wa sheria.

Akizungumzia maadhimisho hayo, Mhe.Hemed amesema yanaakisi hatua kubwa ambazo zimefikiwa katika mageuzi ya sekta ya sheria, hususan matumizi ya teknolojia ya kidijitali yanayolenga kuongeza ufanisi, uwazi na kurahisisha upatikanaji wa huduma za mashtaka kwa wananchi.
Ameeleza kuwa,mifumo ya kidijitali imeendelea kuimarisha misingi ya utawala bora, uwajibikaji na usimamizi wa haki kwa kuhakikisha huduma zinatolewa kwa kuzingatia sheria, uwazi na ufanisi zaidi.

Aidha,amesema matumizi ya teknolojia katika sekta ya sheria yameongeza uwezo wa taasisi za haki katika kupambana na uhalifu wa aina mbalimbali, ikiwemo rushwa, biashara na matumizi ya dawa za kulevya, uhalifu wa kimtandao, uhujumu uchumi, utakatishaji wa fedha pamoja na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia.

Makamu huyo wa Pili wa Rais amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwekeza katika sekta ya sheria na haki kwa kuwa ni msingi muhimu wa maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa, sambamba na utekelezaji wa malengo ya Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar, Ndg. Mgeni Jailani Jecha amesema, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi tangu ilipoanzishwa miaka 24 iliyopita, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati na sheria zinatekelezwa kwa usawa bila ubaguzi.

Amesema,ofisi hiyo imeendelea kusimamia mashitaka ya jinai, kuratibu utekelezaji wa sheria zinazohusu udhibiti na mapambano dhidi ya dawa za kulevya, pamoja na kuanzisha mfumo wa kisasa wa kidijitali wa kufuatilia mwenendo wa kesi mbalimbali, hatua iliyosaidia kuongeza ufanisi katika utoaji wa haki.

Hata hivyo,ameiomba Serikali kuendelea kuiwezesha Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kwa kuipatia gari la kazi litakalorahisisha utekelezaji wa majukumu yake na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Katiba, Sheria,Utumishi na Utawala Bora,Mhe. Dkt. Haroun Ali Suleiman amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi zote zinazounda mnyororo wa utoaji haki ili kuongeza ufanisi wa mfumo wa haki na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati.
Maadhimisho ya miaka 24 ya kuanzishwa kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar yamekuwa fursa ya kutathmini mafanikio yaliyopatikana katika utoaji wa haki, kujadili changamoto zilizopo na kuweka mikakati ya kuendelea kuboresha huduma za mashtaka kupitia matumizi ya teknolojia na ushirikiano wa wadau mbalimbali wa sekta ya sheria.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here