OMO alifanya makusudi kupotosha umma kuhusu mradi wa AFCON-Mbeto

ZANZIBAR-Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis amesema Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman (OMO) aliupotosha umma kuhusu mradi wa ujenzi wa Mji wa Michezo wa AFCON unaojengwa eneo la Fumba, Zanzibar.
Mbeto ametoa kauli hiyo leo Julai 28, 2026 wakati akifafanua mambo mbalimbali, yanayoendelea nchini ikiwemo kauli ya OMO ambaye hivi karibuni wakati akihojiwa na kituo kimoja cha runinga alisema, mradi huo wa AFCON hauna tija, huku akitaja kuwa Serikali imetenga Sh1.6 trilioni kwa ajili ya utekelezaji wake.

Hata hivyo, Mbeto amepinga madai hayo, akisema gharama ya mradi huo ni takribani Sh300 bilioni na kwamba utekelezaji wake hauhusishi ujenzi wa uwanja wa mpira pekee, bali unalenga kuanzisha eneo lenye miundombinu mbalimbali ya michezo, biashara, utalii na huduma nyingine.

Mradi huo unatarajiwa kujumuisha uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu, viwanja vya michezo mbalimbali, hoteli, nyumba za makazi, kumbi za mikutano pamoja na huduma nyingine, ambazo kwa mujibu wa Serikali zitaiwezesha Zanzibar kuwa mwenyeji wa mashindano na matukio makubwa ya kimataifa.

Mbeto amesema,ujenzi wa miundombinu hiyo ni sehemu ya jukumu la Serikali la kuweka mazingira bora ya huduma na maendeleo ya wananchi, akisisitiza kuwa Serikali haiwezi kuachwa bila kuwekeza katika miundombinu ya kisasa kwa hoja kwamba miradi hiyo si biashara ya moja kwa moja.

“Nadhani alifanya makusudi. Yeye si mgeni, anajua uchumi unajengwa vipi, anajua kama kazi ya Serikali si kufanya biashara, ni kutoa huduma na kujenga miundombinu,” amesema Mbeto.

Amesema,Serikali inapaswa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya michezo, barabara na huduma nyingine muhimu kwa kuwa uwekezaji huo una mchango katika kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

Kwa mujibu wa Mbeto, hata OMO angekuwa katika nafasi ya uongozi, angehitajika kufanya uwekezaji kama huo kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi na mwelekeo wa maendeleo ya Zanzibar.

“Huwezi kuwaacha wananchi wako bila kuwajengea miundombinu ya michezo wakati wana historia ya michezo, huwezi kuwaacha wananchi wako wanatembea kwenye barabara mbovu,”amesema.
AFCON na sura mpya ya Zanzibar

Mbeto amesema,mradi huo unapaswa kutazamwa kwa mtazamo mpana zaidi ya matumizi yake wakati wa mashindano ya AFCON, kwa kuwa miundombinu inayojengwa inaweza kutumika kwa shughuli mbalimbali za michezo, mikutano, utalii, biashara na burudani hata baada ya mashindano kumalizika.

Amesema,uwekezaji katika miundombinu ya kisasa ni sehemu ya ushindani wa miji na mataifa katika kuvutia uwekezaji na matukio makubwa ya kimataifa.

Akitoa mifano ya miji iliyowekeza kwa kiwango kikubwa katika miundombinu, Mbeto ametaja Dubai na China, akisema maendeleo ya miji yanachochewa na ujenzi wa barabara, mifumo ya usafiri, majengo na miundombinu ya kisasa.


“Ukienda Dubai au China hakuna majumba mabovu, kila jimbo linalishinda jingine kwa ujenzi wa miundombinu ya barabara, usafiri mbalimbali na majengo ya kisasa,” amesema.

Amesema,Zanzibar haiwezi kuendelea kutumia miundombinu ya zamani bila kufanya maboresho yanayoendana na mahitaji ya sasa, akitolea mfano Uwanja wa Mnazi Mmoja ambao, kwa maelezo yake, hauwezi kutosheleza mahitaji ya michezo ya kisasa.


“Sasa unataka mji uwe vilevile kama ilivyokuwa enzi za mabibi zetu? Au tucheze uwanja uleule wa zamani Mnazi Mmoja wenye michanga na mabonde?,” Alihoji.
Mbeto ampongeza Mwinyi

Katika hatua nyingine, Mbeto amemtaka Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi kuendelea na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa vitendo, akisema Serikali ya Awamu ya Nane imefanya mabadiliko makubwa katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar.

Amesema,uwekezaji unaofanywa katika barabara, michezo na miundombinu mingine ni sehemu ya jitihada za kubadilisha sura ya Zanzibar na kuiweka katika nafasi nzuri zaidi kiuchumi na kijamii.

Kauli ya Mbeto imekuja wakati mjadala kuhusu ujenzi wa Mji wa Michezo wa AFCON Fumba ukiendelea, huku Serikali ikiutazama mradi huo kama sehemu ya maandalizi ya Zanzibar kuwa mwenyeji wa matukio makubwa ya michezo na kimataifa, pamoja na kuongeza miundombinu ya kisasa inayoweza kutumika kwa muda mrefu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here