Onyo kali latolewa dhidi ya utoroshaji wa dhahabu Kahama

KAHAMA-Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda ametoa onyo kali kwa wachimbaji wa madini ya dhahabu, wamiliki wa mialo ya uchenjuaji na wafanyabiashara wa madini hayo kuacha mara moja kujihusisha na biashara haramu ya utoroshaji wa dhahabu, akisisitiza kuwa vitendo hivyo ni kinyume cha sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na Serikali.
Nkinda amesema ni marufuku kwa wachimbaji wenye leseni pamoja na wamiliki wa mialo ya uchenjuaji kuuza dhahabu kwa wanunuzi wasio rasmi maarufu kama makota, ambao wamekuwa wakihusishwa na mtandao wa utoroshaji wa madini.

Akizungumza leo Julai 31,2026 wakati wa kikao elekezi cha utoaji elimu kwa wamiliki wa leseni za uchimbaji, mameneja wa migodi, wamiliki wa mialo ya uchenjuaji na wadau wa sekta ya madini, huku akisoma maazimio 10 ya Kamati ya Usalama ya Wilaya, Nkinda amesema, Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayebainika kushiriki katika biashara haramu ya madini.
Amewataka wadau wote wa sekta hiyo kutunza kumbukumbu sahihi za uzalishaji na mauzo ya madini yao, akionya kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayekiuka sheria.

"Kamati ya Usalama ya Wilaya haitaki kuona migogoro wala vitendo vinavyochochea biashara haramu ya madini. Tunasisitiza kila mmoja afuate sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na Serikali badala ya kutumia njia za mkato,"amesema Nkinda.
Ofisa Mkuu wa Mkoa wa Kimadini wa Kahama,Malembo Chone akiongea kwenye kikao elekezi kwa wachimbaji wa madini wenye leseni, wachejuaji wa dhahabu na mameneja wa migodi, wafanyabishara kuhusu wajibu wao wa kufanya biashara hiyo kwa mjibu wa sheria na kutojihusisha na biashara haramu ya utorishaji wa madini.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Kimadini Kahama, Malembo Chone amesema,bado kuna baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu wanaoendelea kukiuka sheria katika biashara ya madini na kuwataka kuacha na wafanye kazi hiyo kwakufaata sheria.

Amesema,kufuatia matukio ya hivi karibuni ya kukamatwa kwa watuhumiwa wa utoroshaji wa dhahabu jijini Dar es Salaam na mkoani Kagera, ambao baadhi yao walidaiwa kutoka Kahama, ofisi yake imeendesha operesheni maalumu katika migodi na maeneo ya uchenjuaji wa dhahabu na kutoa maelekezo watakao kiuka hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Kwa mujibu wa Chone, operesheni hizo zimebaini kuwepo kwa watu wanaovamia maeneo ya uzalishaji na kujihusisha na ununuzi haramu wa dhahabu kutokana na mwingiliano wa maeneo ya uchimbaji na makazi ya wananchi, huku hatua mbalimbali za kudhibiti vitendo hivyo tayari zikianza kuchukuliwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Dhahabu SHIREMA katika Mgodi wa Mwime, James Sita amesema, wachimbaji wamepokea maelekezo yote yaliyotolewa na Serikali pamoja na Ofisi ya Mkoa wa Kimadini Kahama na kuahidi kuendelea kufanya shughuli zao kwa kuzingatia sheria na miongozo ya Tume ya Madini.

Naye Meneja Masoko wa Kampuni ya Rose, Costa Joseph amesema,kampuni hiyo inaipongeza Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha mazingira ya biashara ya madini nchini.

Ameahidi kuwa kampuni itaendelea kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zote za biashara ya madini ili kuhakikisha rasilimali ya dhahabu inanufaisha wawekezaji, wachimbaji na Taifa kwa ujumla kupitia mapato yanayotokana na sekta hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here