DAR-Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kwa kushirikiana na Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) kimezindua Programu ya Maafisa Waliothibitishwa wa Ulinzi wa Taarifa Binafsi (Certified Data Protection Officer Programme-CDPO Programme) yenye lengo la kuongeza wataalamu wenye uwezo wa kutekeleza majukumu ya uchakataji na ulinzi wa taarifa binafsi kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi,sambamba na kuimarisha uzingatiaji wa sheria hiyo katika taasisi za umma na binafsi nchini.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa programu hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Alex B. Makulilo, amesema mafunzo hayo yanaakisi dhamira ya chuo ya kuendelea kutoa elimu na mafunzo yanayokidhi mahitaji ya taifa katika kukabiliana na changamoto zinazoibuka kutokana na maendeleo ya teknolojia na matumizi ya taarifa binafsi.
Ushirikiano huu utazalisha wataalamu wenye uwezo wa kusimamia na kutekeleza matakwa ya sheria kwa viwango vya kitaifa na kimataifa.
"Katika zama za ukuaji wa teknolojia, taarifa binafsi zimekuwa nguzo muhimu katika sekta mbalimbali, hivyo ni lazima zichakatwe kwa kuzingatia misingi ya kisheria ili kulinda haki za watu binafsi na kuchangia maendeleo ya taifa,"amesema Prof.Makulilo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Dkt. Emmanuel Mkilia, amesema programu hiyo imeanzishwa kwa ushirikiano kati ya taasisi hizi mbili zikiunganisha utaalamu wa kitaaluma na uzoefu wa usimamizi wa sheria, hatua itakayochangia kuwajengea uwezo Maafisa wa Ulinzi wa Taarifa Binafsi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.
"Leo tunaandika historia muhimu katika safari ya Tanzania ya kujenga uchumi wa kidijitali unaozingatia faragha na ulinzi wa taarifa binafsi. Uzinduzi wa programu hii si uzinduzi wa kozi pekee, bali ni mwanzo wa kujenga kizazi cha wataalamu kitakachosimamia ulinzi wa taarifa binafsi nchini kwa uelewa na kuzingatia matakwa ya sheria," amesema Dkt. Mkilia.
Tags
Chuo Kikuu Huria Tanzania
Habari
Open University of Tanzania (OUT)
Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi



