NA DIRAMAKINI
WATAALAMU wa hali ya hewa kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki na Kusini wamekutana jijini Arusha kujadili mikakati ya kuimarisha mifumo ya tahadhari za mapema, hatua inayolenga kuongeza uwezo wa nchi za ukanda huo kukabiliana na athari za majanga yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa na mabadiliko ya tabianchi.
Mkutano huo wa kikanda umewakutanisha wataalamu kutoka Taasisi za Kitaifa za Hali ya Hewa, Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Ofisi ya Hali ya Hewa ya Uingereza (UK Met Office) pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika utoaji wa taarifa za hali ya hewa, kuboresha mifumo ya tahadhari za mapema na kujenga uwezo wa taasisi zinazohusika na huduma za hali ya hewa.
Akifungua mkutano huo kuanzia Julai 13,2026 hadi 17,2026, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Ladislaus Chang'a amesema,mifumo madhubuti ya tahadhari za mapema ni nguzo muhimu katika kupunguza madhara ya majanga ya asili kwa kuwa hutoa taarifa zinazowezesha mamlaka na wananchi kuchukua hatua za tahadhari kabla ya majanga kutokea.
Amesema,uwekezaji katika huduma za hali ya hewa na mifumo ya tahadhari za mapema umeendelea kuwa muhimu kutokana na kuongezeka kwa matukio ya hali mbaya ya hewa yanayohusishwa na mabadiliko ya tabianchi, ambayo yamekuwa yakisababisha mafuriko, ukame, vimbunga na athari nyingine zinazogusa sekta mbalimbali za uchumi.
"Mifumo bora ya tahadhari za mapema inaokoa maisha ya watu, inalinda mali na miundombinu, inapunguza hasara za kiuchumi na kusaidia jamii kufanya maamuzi sahihi kabla na wakati wa matukio ya hali mbaya ya hewa,"amesema Dkt. Chang'a.Ameongeza kuwa,ushirikiano wa kikanda utasaidia kuboresha ubashiri wa hali ya hewa kwa kubadilishana taarifa, uzoefu na teknolojia, jambo litakaloziwezesha nchi wanachama kutoa taarifa sahihi zaidi na kwa wakati kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt.Agnes Kijazi amesema,hakuna nchi inayoweza kukabiliana peke yake na changamoto za mabadiliko ya tabianchi kwa kuwa athari zake huvuka mipaka ya kisiasa na kijiografia.
Amesisitiza kuwa,ushirikiano kati ya nchi za Afrika Mashariki na Kusini ni muhimu katika kuimarisha huduma za hali ya hewa na kuhakikisha taarifa za tahadhari zinawafikia wananchi kwa wakati ili kupunguza madhara ya majanga yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa.
"Mabadiliko ya tabianchi hayana mipaka. Hivyo, ushirikiano wa kikanda na kimataifa ni msingi wa kujenga mifumo madhubuti ya tahadhari za mapema na kuongeza ustahimilivu wa jamii dhidi ya majanga,"amesema Dkt.Kijazi.
Katika mkutano huo, washiriki wanajadili namna ya kuongeza matumizi ya teknolojia za kisasa katika utabiri wa hali ya hewa, kuimarisha uwezo wa Taasisi za Kitaifa za Hali ya Hewa, kuboresha mifumo ya ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa za hali ya hewa pamoja na kuharakisha usambazaji wa tahadhari kwa wananchi na sekta mbalimbali zinazotegemea taarifa hizo.Majadiliano hayo pia yanajikita katika kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana na majanga yanayochochewa na mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo mafuriko, ukame, vimbunga na matukio mengine ya hali mbaya ya hewa ambayo yamekuwa yakiongezeka katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.
Washiriki wanatarajiwa kutoka na mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha ushirikiano wa kikanda, kuongeza uwekezaji katika huduma za hali ya hewa, kuimarisha mifumo ya tahadhari za mapema na kujenga jamii zenye ustahimilivu zaidi dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mkutano huo unaonesha dhamira ya nchi za Afrika Mashariki na Kusini ya kutumia sayansi, teknolojia na ushirikiano wa kikanda kama nyenzo muhimu katika kulinda maisha ya wananchi, mali na uchumi dhidi ya majanga ya hali ya hewa, sambamba na kuchangia utekelezaji wa ajenda ya maendeleo endelevu katika bara la Afrika.
Tags
Habari
Kimataifa
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Tanzania Meteorological Agency (TMA)
Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania
Wataalamu wa Hali ya Hewa

