NA DIRAMAKINI
RAIS wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Mhashamu Wolfgang Pisa, OFMCap, amemteua Padre Profesa Emmanuel Charles Wabanhu kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine Tanzania (SAUT), akichukua wadhifa huo kuanzia Agosti 1, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na SAUT, Mhashamu Pisa ambaye pia ni Kansela wa Chuo Kikuu cha SAUT na Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi, amefanya uteuzi huo ikiwa ni sehemu ya kuendelea kuimarisha uongozi wa taasisi hiyo ya elimu ya juu inayomilikiwa na Kanisa Katoliki Tanzania.
Padre Profesa Wabanhu ni Padri wa Jimbo Katoliki la Geita na Profesa Mshiriki wa Theolojia ya Maadili, akiwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 13 katika ufundishaji, utafiti na uongozi wa kitaaluma katika vyuo vikuu vya ndani na nje ya Tanzania.
Kabla ya uteuzi huo, aliwahi kuhudumu kama Mhadhiri Mwandamizi katika Catholic University of Eastern Africa (CUEA) nchini Kenya.
Pia aliwahi kuwa Naibu Mkuu wa Chuo anayesimamia Utawala na Fedha katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mihayo (AMUCTA) nchini Tanzania, ambako alisimamia masuala ya utawala wa taasisi na usimamizi wa rasilimali.
Mbali na uzoefu wake wa kiuongozi, Padre Profesa Wabanhu amejijengea sifa katika utafiti na uchapishaji wa kazi za kitaaluma.
Ameandika vitabu vitano na kuchapisha zaidi ya makala 20 za kisayansi katika majarida ya kimataifa yanayotambuliwa, mchango unaodhihirisha umahiri wake katika taaluma ya theolojia na maadili.
Katika upande wa elimu, Padre Profesa Wabanhu ana Shahada ya Kwanza ya Theolojia kutoka Pontifical Urban University ya Roma, Italia.
Aidha, ana Shahada mbili za Uzamili, Shahada ya Uzamivu wa Theolojia (STD) pamoja na Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Maadili ya Jamii na Biashara kutoka Katholieke Universiteit Leuven nchini Ubelgiji.
Uteuzi wake unatarajiwa kuimarisha dhamira ya SAUT ya kuendelea kutoa elimu ya juu yenye ubora, kuendeleza tafiti na ubunifu, pamoja na kukuza maadili na uongozi unaozingatia misingi ya kitaaluma na huduma kwa jamii.
SAUT ni miongoni mwa vyuo vikuu vikuu vinavyomilikiwa na Kanisa Katoliki nchini Tanzania, kikitoa programu mbalimbali za elimu ya juu katika ngazi za shahada, uzamili na uzamivu, huku kikichangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya rasilimali watu nchini.
Tags
Bishop Wolfgang Pisa
Habari
Kanisa Katoliki Tanzania
Padre Profesa Emmanuel Charles Wabanhu
SAUT University
