Profesa Nagu aridhishwa na huduma zinazotolewa katika banda jumuishi la Ofisi ya Waziri Mkuu ndani ya Sabasaba

DAR-Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Afya katika Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI, Prof. Tumaini Nagu ametembelea Banda Jumuishi la Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba 2026) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, na kupongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Akiwa katika ziara hiyo, Prof. Nagu amepata fursa ya kutembelea sehemu mbalimbali za banda hilo na kupokea maelezo kuhusu huduma na mifumo mbalimbali inayowezesha wananchi kupata taarifa na huduma zinazotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na taasisi zake.

Amesema,banda hilo limekuwa jukwaa muhimu la kuwaelimisha wananchi kuhusu utekelezaji wa programu na miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha utoaji wa huduma za kijamii, hususan katika sekta ya afya, elimu, utawala bora na maendeleo ya serikali za mitaa.

Prof. Nagu amewapongeza watumishi wanaohudumu katika banda hilo kwa kujituma, kutoa elimu kwa ufasaha na kuhakikisha kila mwananchi anayefika anapata huduma na taarifa sahihi zinazomwezesha kufahamu shughuli zinazotekelezwa na Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu.
Aidha, amewataka kuendelea kutumia maonesho hayo kama fursa ya kusikiliza maoni ya wananchi, kupokea changamoto zao na kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu huduma zinazotolewa, ili kuongeza uelewa na kuimarisha uhusiano kati ya Serikali na wananchi.

"Banda Jumuishi la Ofisi ya Waziri Mkuu limeendelea kuvutia maelfu ya wananchi wanaotembelea Maonesho ya Sabasaba, ambapo wamekuwa wakipata elimu na huduma mbalimbali zinazotolewa na Ofisi hii pamoja na taasisi zake kwa lengo la kuboresha ustawi wa wananchi na kuharakisha maendeleo ya Taifa, hivyo wananchi endeleeni kuitumia fursa ya uwepo wa ofisi hii katika maonesho haya,"amesema Dkt.Nagu.
Aidha,ametumia nafasi hiyo kuipongeza Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) pamoja na Taasisi nyingine zilizowezesha mafanikio ya maonesho hayo huku akiiasa jamii kuendelea kutembelea banda hilo na kupata elimu.

Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanaendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere chini ya kaulimbiu isemayo, "Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba ni Fahari ya Tanzania," yakilenga kukuza biashara, uwekezaji na ubunifu nchini.
Miongoni mwa Taasisi za Ofisi ya Waziri Mkuu zilizoshiriki ni pamoja na PSSSF, WCF, NSSF, OSHA, NEEC, TNBC, CMA, TACAIDS, DCEA,Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, DART, TARURA, Chuo cha Serikali za Mitaa (LGTI) pamoja na Shirika la Masoko Kariakoo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here