RUKWA-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Silas Shemdoe, amewasili mjini Sumbawanga kwa ajili ya kumuwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, katika ufunguzi wa mafunzo ya utoaji elimu kuhusu fursa za mitaji na huduma za uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.
Mafunzo hayo yatafanyika kuanzia Julai 13 hadi 16, 2026 katika Manispaa ya Sumbawanga, yakiwa yameratibiwa na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Rukwa, Mhe. Jacqueline Mzindakaya, kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).
Prof. Shemdoe alipokelewa katika Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Makongoro Nyerere akiambatana na Mhe. Mhe. Jacqueline Mzindakaya pamoja na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali.Kesho, Julai 13, 2026, Prof. Shemdoe atafungua rasmi mafunzo hayo katika Ukumbi wa Country Hotel, ambapo yanatarajiwa kuwakutanisha wananchi, wajasiriamali, vikundi vya wanawake na vijana, makundi yenye mahitaji maalum pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea wananchi uelewa kuhusu fursa za mitaji, mikopo na huduma mbalimbali za uwezeshaji zinazotolewa na Serikali na taasisi zake, ili kuongeza ushiriki wao katika shughuli za uzalishaji, kukuza biashara, kuongeza ajira na kuinua kipato cha familia.
Mafunzo hayo pia yanatarajiwa kuwapa washiriki taarifa sahihi kuhusu namna ya kufikia huduma za kifedha na programu za uwezeshaji wa kiuchumi, hatua itakayochochea ukuaji wa uchumi wa wananchi na kuharakisha maendeleo ya mkoa wa Rukwa kwa ujumla.










