ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano na mawasiliano baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ili kuimarisha na kuendeleza maslahi ya wananchi.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Julai 30, 2026 alipokutana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Ndg. Charles Ngeleja Kadonya, aliyefika kwa mazungumzo ya kikazi kufuatia uteuzi wake katika wadhifa wake mpya.
Amesema ushirikiano na mawasiliano yaliyoimarika baina ya pande mbili za Muungano yamechangia kutatuliwa kwa changamoto mbalimbali zilizodumu kwa muda mrefu na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa masuala yenye maslahi ya pamoja.
Rais Dkt. Mwinyi ameitaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuhakikisha Zanzibar inashirikishwa ipasavyo katika majadiliano na mipango ya miradi ya maendeleo ya kikanda, ili iweze kunufaika kikamilifu na fursa zinazopatikana kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki.Aidha, ameeleza kuridhishwa na ushirikiano uliopo baina ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, huku akisisitiza umuhimu wa kuuendeleza ili kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuleta manufaa zaidi kwa wananchi.
Rais Dkt. Mwinyi amemtakia Ndg. Kadonya mafanikio katika utekelezaji wa majukumu yake mapya, huku akimweleza umuhimu wa kuendeleza mawasiliano ya karibu na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Kwa upande wake, Bw. Kadonya amemhakikishia Rais Dkt. Mwinyi kuwa ataendelea kuimarisha ushirikiano baina ya Wizara hiyo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, pamoja na kusimamia maslahi ya Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

