Rais Dkt.Mwinyi kuelekea nchini India kwa ziara ya kikazi

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi anatarajiwa kuondoka Zanzibar tarehe 16 Julai 2026 kuelekea Jamhuri ya India kwa ziara ya kikazi ya siku tatu, itakayoanzia tarehe 17 hadi 19 Julai 2026, kufuatia mwaliko rasmi wa Makamu wa Rais wa India, Mhe.Shri C. P. Radhakrishnan.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Julai 15,2026 na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu ya Zanzibar,Raqey Mohamed.

Katika ziara hiyo, Rais Dkt. Mwinyi ataambatana na ujumbe wake, akiwemo Mke wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Mama Mariam Mwinyi, pamoja na viongozi mbalimbali.

Pia, kwa mujibu wa taarifa hiyo, ziara hiyo inalenga kuendeleza na kuimarisha uhusiano wa kihistoria na wa kirafiki baina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya India katika nyanja mbalimbali, zikiwemo elimu, biashara, uwekezaji, afya, sayansi, teknolojia, utamaduni na uhusiano baina ya wananchi wa pande zote mbili.

Akiwa jijini Chennai, Rais Dkt. Mwinyi anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika Mahafali ya 63 ya Taasisi ya Teknolojia ya India Madras (IIT Madras), yatakayofanyika tarehe 17 Julai 2026.

Ushiriki wake katika mahafali hayo unaakisi ushirikiano wa kipekee katika sekta ya elimu baina ya Zanzibar na taasisi hiyo, ulioimarishwa kupitia kuanzishwa kwa Kampasi ya IIT Madras Zanzibar, ambayo ni kampasi ya kwanza ya taasisi hiyo kuanzishwa nje ya India.

Rais Dkt. Mwinyi pia anatarajiwa kuzungumza na viongozi wa IIT Madras kuhusu maeneo ya kimkakati ya ushirikiano, pamoja na kutembelea maabara na vituo vya utafiti, ubunifu na teknolojia.

Katika maeneo hayo, atapata fursa ya kujionea namna India inavyounganisha elimu ya juu, utafiti, teknolojia, uzalishaji viwandani na maendeleo ya biashara bunifu.

Katika ziara hiyo, Mke wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Mama Mariam Mwinyi, anatarajiwa kushiriki mkutano maalumu wa Jukwaa la Wanawake la IIT Madras, jijini Chennai.

Mkutano huo utajadili uongozi, elimu na uwezeshaji wa wanawake, pamoja na kubadilishana uzoefu kuhusu mikakati inayotekelexwa Zanzibar na India ili kuongeza ushiriki wao katika uongozi na maendeleo ya jamii.

Akiwa New Delhi, Rais Dkt. Mwinyi anatarajiwa kuzungumza na Makamu wa Rais wa India, Mhe. Shri C. P. Radhakrishnan, pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Dkt. S. Jaishankar, kuhusu kuimarisha ushirikiano wa kisiasa, kidiplomasia na kiuchumi, utekelezaji wa miradi ya pamoja na kuibua fursa mpya za ushirikiano katika sekta mbalimbali, hususan elimu, teknolojia, afya, biashara na uwekezaji baina ya nchi hizo mbili.

Ziara hiyo inatarajiwa kufungua fursa mpya za ushirikiano, kuvutia uwekezaji, kuimarisha diplomasia ya uchumi na kuongezeana maarifa, teknolojia na uzoefu.

Aidha, itaendeleza dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuifanya Zanzibar kuwa kitovu cha elimu, utafiti, ubunifu na teknolojia katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Rais Dkt. Mwinyi anatarajiwa kurejea nchini tarehe 20 Julai 2026, baada ya kukamilisha ziara hiyo ya kikazi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here