NA DIRAMAKINI
SERIKALI ya Msumbiji imesema inatarajia kampuni ya mafuta na gesi ya Marekani, ExxonMobil kufanya uamuzi wa mwisho wa uwekezaji (Final Investment Decision-FID) kwa mradi mkubwa wa gesi asilia iliyoyeyushwa (LNG) katika Mkoa wa Cabo Delgado mwezi Septemba mwaka huu, hatua inayotarajiwa kufungua njia ya utekelezaji wa moja ya miradi mikubwa zaidi ya uwekezaji binafsi barani Afrika.


Picha na Mtandao.
Rais wa Msumbiji,Daniel Chapo amesema, mazungumzo kati ya Serikali na ExxonMobil yanaendelea vizuri na kwamba endapo kila kitu kitaenda kama kilivyopangwa, pande hizo zitafikia uamuzi wa mwisho wa uwekezaji mwezi Septemba 2026.
"Tunaendelea vizuri katika mazungumzo na ExxonMobil. Endapo kila kitu kitaenda kama ilivyopangwa, mwezi Septemba mwaka huu tutafanya uamuzi wa mwisho wa uwekezaji. Huu ni mradi mkubwa zaidi wa uwekezaji binafsi barani Afrika wenye thamani ya takribani dola bilioni 20 za Marekani,"amesema Rais Chapo katika mahojiano na Shirika la Habari la Ureno (Lusa) kabla ya kuanza ziara rasmi ya siku nne nchini Ureno.
Mradi wa Rovuma LNG, unaoongozwa na ExxonMobil unatarajiwa kujengwa katika Mkoa wa Cabo Delgado na kutumia baadhi ya miundombinu kwa pamoja na mradi jirani wa TotalEnergies LNG, ambao umeanza tena kutekelezwa baada ya kusimamishwa kwa takribani miaka mitano kutokana na mashambulizi ya kigaidi yaliyolikumba eneo hilo mwaka 2021.
Mnamo Januari 26,2026 wakati wa hafla ya kurejelewa kwa shughuli za mradi wa TotalEnergies katika eneo la Afungi, Rais Chapo alieleza kuwa,mradi wa ExxonMobil unatarajiwa kuanza ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuharakisha matumizi ya rasilimali za gesi asilia kwa maendeleo ya uchumi wa taifa.
ExxonMobil ilitangaza Novemba 20,mwaka jana kuwa imeondoa rasmi tamko la kufanya maamuzi magumu (force majeure) lililokuwa limezuia utekelezaji wa mradi huo kufuatia hali ya usalama katika Mkoa wa Cabo Delgado.
Hatua hiyo imefungua njia kuelekea kufikiwa kwa uamuzi wa mwisho wa uwekezaji unaotarajiwa mwezi Septemba,mwaka huu.
Mradi wa Rovuma LNG ni miongoni mwa miradi mikubwa zaidi ya gesi asilia barani Afrika na unalenga kuzalisha tani milioni 18 za gesi asilia iliyoyeyushwa (LNG) kwa mwaka kutoka Kitalu Na. 4 katika Bonde la Rovuma.
Kwa upande mwingine, mradi wa Area 1 LNG unaoongozwa na kampuni ya TotalEnergies unatarajiwa kuanza kusafirisha LNG mwaka 2029 ukiwa na uwezo wa kuzalisha tani milioni 13 kwa mwaka.
Aidha, kampuni ya Eni ya Italia tayari imeanza uzalishaji wa LNG kupitia jukwaa la baharini la Coral Sul tangu mwaka 2022.
Kampuni hiyo pia imeidhinisha uwekezaji wa dola bilioni 7.2 katika mradi wa Coral Norte, ambao unatarajiwa kuanza uzalishaji mwaka 2028 na kuongeza uwezo wa uzalishaji hadi tani milioni saba kwa mwaka, huku mipango ya kuendeleza jukwaa la tatu ikiendelea.
Miradi hiyo mitatu ya gesi asilia inaifanya Msumbiji kuwa miongoni mwa nchi zenye matarajio makubwa ya kuwa kitovu cha uzalishaji na usafirishaji wa gesi asilia iliyoyeyushwa duniani, kutokana na akiba kubwa ya gesi iliyopo katika Bonde la Rovuma, linalotajwa kuwa miongoni mwa maeneo yenye hifadhi kubwa zaidi za gesi duniani.
Serikali ya Msumbiji ina matumaini kuwa utekelezaji wa miradi hiyo utaongeza mapato ya taifa, kuvutia uwekezaji wa kimataifa, kuzalisha ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi katika miaka ijayo, huku ikisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha usalama katika Mkoa wa Cabo Delgado ili kuhakikisha uwekezaji huo unatekelezwa kwa mafanikio.