Rais Dkt.Samia azindua meli nne,aweka jiwe la msingi ujenzi wa SGR kipande cha sita Tabora hadi Kigoma

KIGOMA-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan leo amezindua meli nne mpya za mizigo katika Ziwa Tanganyika na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha Tabora hadi Kigoma, yenye urefu wa kilomita 506.
Rais Dkt. Samia amesema Serikali inaendelea kujenga mfumo jumuishi wa uchukuzi nchini unaounganisha reli, bandari, barabara na viwanja vya ndege ili kupunguza gharama za usafirishaji, kuongeza ushindani wa biashara na kufungua masoko mapya.

"Kigoma haitakuwa tena mwisho wa reli. Itakuwa mwanzo wa kufunguka kwa fursa za
biashara na uwekezaji," amesema Rais Dkt. Samia.

Ameongeza kuwa, reli ya Tabora–Kigoma, itakapokamilika, itaunganisha mkoa huo na Bandari ya Dar es Salaam pamoja na mtandao wa bandari za kisasa katika Ziwa Tanganyika, hivyo kurahisisha usafirishaji wa mizigo ndani na nje ya nchi.
Rais Dkt. Samia amesema uwekezaji unaoendelea kufanywa na Serikali utafungua fursa mpya za ajira katika reli, bandari, maghala, usafirishaji, hoteli na huduma nyingine za ugavi.

Miradi hiyo pia, amesema Rais Dkt. Samia, itawanufaisha wakazi wa Mkoa wa Kigoma, hususan wakulima na wavuvi, kwa kuwezesha usafirishaji wa haraka, nafuu na wa uhakika wa pembejeo, mazao yao, pamoja na kupunguza muda na gharama za usafirishaji.

Vilevile, Rais Dkt. Samia ameielekeza Wizara ya Uchukuzi kushirikiana na sekta binafsi kusimamia ujenzi wa karakana ya kisasa ya matengenezo ya meli mkoani Kigoma.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amesema, ujenzi wa meli hizo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kupanua huduma za usafiri wa majini katika Ziwa Tanganyika, kwa kushirikiana na sekta binafsi.

Waziri Mbarawa amesema Serikali imedhamiria kuwa na jumla ya meli 14 mpya ifikapo mwaka 2028, hatua itakayoongeza uwezo wa usafirishaji wa mizigo, kuchochea biashara na kuvutia uwekezaji zaidi katika ukanda wa Maziwa Makuu.
Naye, Makamu wa Rais wa kampuni, iliyojenga meli hizo, ya Zhiji Mining Group, Bw. Qiu Guozhu, amesema kampuni hiyo itaendelea kuwekeza katika uboreshaji wa Bandari ya Kigoma na miundombinu ya usafirishaji ili kuongeza ufanisi wa biashara ya kikanda.

Ameongeza kuwa mradi wa ujenzi wa meli nne za mizigo unaakisi ushirikiano unaoendelea kuimarika kati ya Tanzania na China.

“Mradi huu ni ushahidi wa urafiki unaoendelea kuimarika na ushirikiano wa vitendo kati
ya China na Tanzania,” amesema Guozhu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here