Rais wa CAF Dkt.Patrice Motsepe aomboleza kifo cha nyota wa Bafana Bafana,Jayden Adams

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), Dkt. Patrice Motsepe ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha kiungo wa kimataifa wa Afrika Kusini na klabu ya Mamelodi Sundowns, Jayden Adams kilichotokea akiwa na umri wa miaka 25.
Katika taarifa iliyotolewa na Idara ya Mawasiliano ya CAF, Dkt.Motsepe amesema, kifo cha Adams ni pigo kubwa kwa familia ya soka nchini Afrika Kusini na barani Afrika, akieleza kuwa mchezaji huyo alikuwa miongoni mwa vipaji vilivyokuwa vikitarajiwa kuendelea kung'ara katika soka la kimataifa.

Kwa niaba ya CAF na Vyama vya Soka 54 wanachama wake, Dkt. Motsepe alitoa salamu za pole kwa Chama cha Soka Afrika Kusini (SAFA), Rais wake Dkt.Danny Jordaan, klabu ya Mamelodi Sundowns pamoja na familia ya marehemu Jayden Adams.

Adams alikuwa sehemu ya kikosi cha Bafana Bafana kilichoshiriki fainali za Kombe la Dunia la FIFA 2026, hatua iliyodhihirisha maendeleo yake makubwa katika soka la kimataifa na kumweka miongoni mwa wachezaji muhimu wa kizazi kipya cha Afrika Kusini.

Mbali na mafanikio yake katika timu ya taifa, Adams pia alikuwa sehemu ya kikosi cha Mamelodi Sundowns kilichotwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika ya TotalEnergies CAF 2026, baada ya ushindi katika fainali zilizofanyika mjini Rabat, Morocco. Mafanikio hayo yaliongeza hadhi yake kama mmoja wa viungo bora waliokuwa wakichipukia barani Afrika.

Kabla ya kujiunga na Mamelodi Sundowns, Adams alichezea Stellenbosch FC, ambako alijizolea sifa kutokana na kiwango chake bora kilichomwezesha kupata nafasi ya kuitumikia timu ya taifa ya Afrika Kusini. Kupitia uwezo wake wa kucheza katikati ya uwanja, alikuwa ameanza kujijengea nafasi ya kudumu katika kikosi cha Bafana Bafana.

Kifo chake kimeacha pengo kubwa katika soka la Afrika Kusini na bara la Afrika kwa ujumla, huku wadau wa mchezo huo wakiendelea kutoa salamu za pole na kumuenzi kwa mchango wake ndani na nje ya uwanja.

Dkt.Motsepe ameiombea familia ya marehemu nguvu katika kipindi hiki kigumu na kumuombea Jayden Adams apumzike kwa amani.

"Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Jayden Adams mahali pema peponi."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here