DAR-Waziri Mkuu Dkt.Mwigulu Nchemba amesema Serikali imepokea ombi la Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) la kutoa fursa ya mikopo kwa vijana wanaosoma kozi za muda mfupi kwenye chuo hicho.
"Mkuu wa Chuo ulieleza uwepo wa hii changamoto ukisisitiza kwamba ukosefu wa mikopo unafanya idadi ya wanafunzi ipungue kwani watoto wa matajiri ndiyo wanaweza kusoma kwa kuwa wanamudu ada hizo,” amesema.
“Kozi hii inahitaji utimamu wa akili bila kujali mwanafunzi anatoka kwenye familia ipi. Mheshimiwa Rais wetu amejitambulisha kwa kutoa Samia Scholarship kwa wanafunzi wanaofanya vizuri na kupata ufaulu wa juu.
"Kigezo siyo mwanafunzi ametoka kwenye familia ipi bali ufaulu wake wa kidato cha sita kwa kupata alama tatu za A,” amesema Waziri Mkuu.
Ametoa kauli hiyo leo Julai 30,2026 wakati akizungumza na washiriki wa Kongamano la Chama cha Wataalamu wa Lojistiki na Usafirishaji Tanzania la Mwaka 2026 lililofanyika kwenye Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Mabibo, jijini Dar es Salaam.
Ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji wa sh. bilioni 70 kwenye chuo hicho. “Kupitia uwekezaji huo, nimejionea uwekezaji mkubwa unaofanyika kwenye miundombinu ya mabweni na ya kujifunzia,”amesisitiza.
Akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa kongamano hilo, Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile alisema kuwa sekta ya uchukuzi ni kiungo muhimu katika ukuaji wa uchumi ambapo kwa mwaka wa fedha uliopita sekta hiyo imechangia katika pato la Taifa kwa takribani dola za Marekani bilioni 2.8.
Mapema, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alisema kuwa Serikali imetoa fedha kujenga kituo cha usafirishaji wa anga kwenye chuo hicho kwa kutoa sh. bilioni 15 za kununua ndege tano za mafunzo kwa ajili ya marubani, mafundi na wahudumu wa ndege pamoja na waongoza ndege.
“Vilevile, Serikali imetoa sh. bilioni mbili ambao zimetumika kujenga barabara za lami ndani ya chuo hicho. Umetembea hapa bila kupata vumbi,” amesema.
Naye, Mkuu wa Chuo hicho, Dkt. Prosper Mgaya alisema chuo hicho ni cha pili barani Afrika kikifuatia Ethiopian Aviation Academy lakini pia ni cha kwanza katika nchi za Afrika Mashariki. Alisema kimejipanga kutoa mafunzo ambayo yatatoa fursa za ajira kwa Watanzania hadi nje ya nchi.
“Kupitia mafunzo haya, tumetoa mafundi wa aircraft maintanance ambao wamepata ajira ATCL na Air Dubai. Kupitia mafunzo ya vitendo, tumesajili wanafunzi wa urubani 22. Lakini pia tayari marubani wanne wamehitimu na wanane wanaruka solo (bila uangalizi na hivyo wako tayari kuingia sokoni).”












