Serikali yaahidi kupeleka shilingi milioni 700 kuiwezesha Hospitali ya Ifakara kutoa huduma ya kulaza wagonjwa

MOROGORO-Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ifakara wanatarajia kunufaika na huduma za kulaza wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya ya Ifakara mara baada ya Serikali kuahidi kutoa Shilingi Milioni 700 ndani ya mwezi Julai, 2026 kwa ajili ya kukamilisha miundombinu muhimu itakayowezesha hospitali hiyo kuanza kutoa huduma hiyo kwa wagonjwa.
Ahadi hiyo ya Serikali imetolewa na Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Julai 6, 2026 akiwa kata ya Kiberege, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo, ambapo alipokea taarifa za utekelezaji wa miradi ya nyumba nne za Wakuu wa Idara, majengo matatu ya Hospitali ya Wilaya na Soko la Kiberege na kuweka mawe ya msingi katika miradi hiyo.

Prof. Shemdoe amesema Serikali itapeleka Shilingi Milioni 700 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa jengo la utawala, chumba cha kuhifadhia maiti pamoja na njia za kupita (walkways) katika Hospitali ya Wilaya ya Ifakara, ili kuwezesha hospitali hiyo kuanza rasmi huduma za kulaza wagonjwa na kupunguza adha iliyokuwa ikiwakabili wananchi kutafuta huduma hizo mbali na maeneo yao.
Prof. Shemdoe amefafanua kuwa, fedha hizo zinaakisi dhamira ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kuimarisha huduma za afya na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora karibu na makazi yao na kuongeza kuwa, wananchi wanapaswa kuendelea kulinda amani na utulivu uliopo ili Serikali iendelee kutekeleza miradi ya maendeleo kwa manufaa ya umma na taifa.

"Fedha hizi ni ishara ya upendo wa Rais Samia kwa wananchi wa Ifakara. Anawapenda na ameazimia kuona huduma za afya zinaboreshwa na maisha ya wananchi yanabadilika kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo," amesema Prof. Shemdoe.

Mbali na sekta ya afya, Prof. Shemdoe amesema Serikali itatoa Shilingi Milioni 330 kwa ajili ya ujenzi wa Daraja la Mkasu kama ilivyotoa Shilingi Milioni 191 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa soko la Kiberege, miradi inayolenga kuboresha huduma ya usafiri na usafirishaji, biashara pamoja na kuinua uchumi wa wananchi.

Akizungumzia utekelezaji wa ujenzi wa barabara zenye urefu kilomita 10, Prof. Shemdoe amemuelekeza Mhe. Sultan Kwanja, Diwani wa Kata ya Kiberege kuweka kipaumbele katika ujenzi wa barabara zinazoelekea kwenye maeneo yenye shughuli za kilimo ili kurahisisha usafirishaji wa mazao na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mhe. Adam Malima, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, amesema ziara ya Mhe. Prof. Shemdoe imelenga kutatua changamoto za wananchi na si kufanya ziara zenye mlengo wa kuwahadaa wananchi.
"Waziri wa TAMISEMI hajaja kufanya sanaa; amekuja kushughulikia changamoto za wananchi, ndiyo maana aliposikia changamoto ya barabara ameambatana na Meneja wa TARURA Mkoa wa Morogoro pamoja na Meneja wa TARURA Wilaya ya Ifakara ili kuhakikisha suala hilo linapatiwa ufumbuzi," amesema Mhe. Malima.

Naye, Mhe. Abubakari Asenga, Mbunge wa Jimbo la Ifakara, amewahakikishia wananchi kuwa ujenzi wa barabara za mitaa utasimamiwa kwa karibu chini ya uongozi wa Prof. Shemdoe, akibainisha kuwa mafanikio yaliyopatikana katika upatikanaji wa fedha za soko la Kiberege yanaonesha dhamira ya Serikali ya kutekeleza pia miradi mingine ya maendeleo.

Akiwa wilayani Ifakara, Prof. Shemdoe amekagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo nyumba nne za wakuu wa idara, majengo matatu ya hospitali ya wilaya ya Ifakara na soko la Kiberege, ikiwa ni pamoja na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here