Sheria ina thamani pale inapobadilisha maisha ya watu-Mwanasheria Mkuu wa Serikali

DAR-Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S.Johari amesema kuwa, Sheria zinapaswa kutumika kama nyenzo ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kufungua fursa, kuongeza uwajibikaji, kuvutia uwekezaji, kuongeza mapato ya Serikali, kuboresha elimu na afya.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameyasema hayo, wakati wa Uzinduzi wa Kitabu kipya kiitwacho " Falsafa ya Sheria ya Mama Samia: Utekelezaji wake katika Mageuzi ya Kiuchumi na Kijamii, ulioratibiwa na Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzani n kufanyika katika Ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Julai 10, 2026.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesisitiza kuwa,thamani ya Sheria hupimwa kwa uwezo wake wa kuboresha maisha ya wananchi, kuvutia uwekezaji,kuimarisha uwajibikaji na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa Wananchi.

Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameeleza kuwa, wazo la kuandika kitabu hicho lilitokana na tafakuri ya kina kuhusu nafasi ya sheria katika kuchochea maendeleo, ambapo waandishi wa Kitabu hicho walitaka kujibu maswali muhimu kuhusu namna marekebisho ya sheria, mabadiliko ya sera na maboresho ya taasisi yalivyochangia kuleta matokeo chanya katika uchumi na ustawi wa jamii.

"Kitabu hiki hakikuandikwa kwa lengo la kusifu tu mazuri yaliyofanyika, , bali ni hii kazi ya uchambuzi wa kitaaluma inayotumia ushahidi, takwimu na nyaraka rasmi kuchunguza kama mageuzi ya kisheria na kisera yaliyofanyika tangu Machi mwaka 2021 yanaonesha mfumo unaoweza kueleweka, kupimwa na kujadiliwa kitaaluma,"amesema Mhe. Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mhe. Johari amefafanua kuwa, lengo kuu lilikuwa kuhamisha mjadala kutoka kwenye kauli za jumla kwenda kwenye ushahidi wa kisayansi kwa kuangalia matokeo halisi ya marekebisho ya sheria na sera kwa wananchi.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, amesema pia kuwa kitabu hicho kinaonesha kuwa katika kipindi cha Awamu ya Sita kumekuwa na mwelekeo mpya wa kutumia sheria, sera, taasisi na mifumo ya utekelezaji kujenga mazingira ya maridhiano, uwekezaji, uwazi, haki,utoaji huduma bora na maendeleo ya wananchi.

"Ndiyo maana tuliona ni muhimu kuuweka mwelekeo huu katika maandishi ili uwe rejea kwa watunga sera, wasomi, watafiti na wadau wengine wanaotaka kuelewa nafasi ya sheria katika maendeleo ya taifa,"amesema.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa kwa mujibu wa majukumu ya kikatiba ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ushauri wa kisheria haupaswi kuishia katika tafsiri ya sheria pekee, bali unapaswa kusaidia Serikali kufanya maamuzi yanayolinda maslahi ya taifa, kupunguza migogoro, kuvutia uwekezaji na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Sheria nzuri zinapaswa kuwa wazi, zenye mantiki, zinazotekelezeka na zinazotabirika, huku zikitoa mazingira rafiki kwa ukuaji wa uchumi na kuimarisha taasisi za umma,"amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Katika hatua nyingine Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaendelea kusimamia ubora wa utungaji wa sheria, usimamizi wa mikataba ya Serikali, matumizi ya mifumo ya kidijitali katika huduma za kisheria pamoja na kujenga uwezo wa mawakili wa Serikali ili waendane na mabadiliko ya uchumi, teknolojia na mazingira ya kimataifa.

“Sheria ina thamani pale inapoboresha maisha ya watu, kuvutia uwekezaji, kuongeza mapato ya Serikali, kuboresha elimu na afya, kupanua upatikanaji wa nishati, kulinda taarifa binafsi, na kupunguza migogoro,"amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Vilevile, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake ambao umekuwa chachu kwa maendeleo ya nchi.

“Napenda kutumia nafasi hii kutoa shukrani za dhati kwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuongoza nchi kwa mwelekeo wa maridhiano, mageuzi, ustawi na maendeleo,”amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Sambamba na hilo, Mhe. Johari amewapogeza na kuwashukuru waandishi, wahakiki, wahariri, Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania, Wizara ya Katiba na Sheria, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na wadau wote waliofanikisha kupatikana kwa kitabu hicho.

Kitabu cha Falsafa ya Sheria ya Mama Samia kinakusudia kuwa rejea muhimu sana kwa Serikali, wasomi, watafiti, mawakili, sekta binafsi na wadau wengine katika kuendeleza mjadala kuhusu nafasi ya sheria kama nguzo ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here