KAMPALA-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba amesema,uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika licha ya changamoto za uchumi wa dunia, ukikua kwa asilimia 5.9 mwaka 2025 na unatarajiwa kufikia asilimia 6.3 mwaka 2026.
Akizungumza katika Mkutano wa 29 wa Kamati ya Masuala ya Fedha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (MAC) uliofanyika Julai 24, 2026 jijini Kampala nchini Uganda, Gavana Tutuba amesema, mfumuko wa bei umeendelea kubaki ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5, ukifikia asilimia 4.0 mwezi Juni 2026 baada ya kupanda hadi asilimia 4.2 mwezi Mei kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta duniani.Amesema,Benki Kuu iliongeza Kiwango Kikuu cha Riba (CBR) kutoka asilimia 5.75 hadi 6.25 ili kudhibiti shinikizo la mfumuko wa bei.
Aidha, amesema nakisi ya urari wa akaunti ya sasa iliongezeka kidogo hadi asilimia 2.4 ya Pato la Taifa katika mwaka ulioishia Juni 2026 kutokana na misukosuko ya nje, huku akiba ya fedha za kigeni ikizidi dola za Marekani bilioni 6, zinazotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kwa miezi 4.5.Aliongeza kuwa,akiba ya kimataifa ikijumuisha dhahabu ambayo bado haijageuzwa kuwa akiba ya fedha imefikia takribani dola za Marekani bilioni 8.7.
Kwa upande wa sera za fedha za Serikali, alisema nakisi ya bajeti inakadiriwa kushuka hadi asilimia 3.1 ya Pato la Taifa mwaka 2025/26, wakati deni la umma linaendelea kuwa himilivu likiwa asilimia 39.6 ya Pato la Taifa, chini ya kiwango cha asilimia 50 kilichowekwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Gavana Tutuba alisema sekta ya fedha nchini imeendelea kuwa imara na salama, huku kiwango cha mikopo chechefu kikishuka hadi asilimia 2.9 kutoka asilimia 12.5 mwaka 2017.
Alisisitiza kuwa Benki Kuu itaendelea kutekeleza mageuzi ya kuimarisha uthabiti wa sekta ya fedha na kushirikiana kwa karibu na taasisi nyingine za kikanda katika kuendeleza ajenda ya ushirikiano na kufanikisha malengo ya pamoja ya maendeleo ya uchumi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

