TANGA-Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Mheshimiwa Balozi Dkt.Batilda Salha Burian amekabidhiwa tuzo maalumu na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ikiwa ni kutambua mchango wake katika kuimarisha utawala wa sheria na usimamizi wa haki mkoani humo.
Tuzo hiyo imekabidhiwa leo Julai 27,2026 na Wakili wa Serikali Mkoa wa Tanga, Bi.Rebecca Msalangi baada ya kumtembelea Mkuu huyo ofisini kwake jijini Tanga.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, tuzo hiyo imetolewa kwa kutambua mchango mkubwa wa Mhe. Burian katika kufanikisha uzinduzi wa Kamati ya Ushauri wa Kisheria Mkoa wa Tanga pamoja na ushirikiano wake wa karibu na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kuhakikisha migogoro ya wananchi inashughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi kwa wakati.
Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wananchi kwa njia ya ushirikiano kati ya viongozi wa Serikali na taasisi za sekta ya sheria.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mhe. Burian ameipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuendelea kuimarisha sekta ya sheria kupitia ubunifu mbalimbali, ikiwemo uandishi wa Kitabu cha Falsafa ya Sheria ya Mama Samia (Mama Samia Doctrine of Law).
Amesema, kitabu hicho kinaakisi kwa kina maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha utawala wa sheria kama nguzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kiutawala nchini.
Balozi Burian ameeleza kuwa, falsafa hiyo imeendelea kutoa mwelekeo wa kujenga taasisi zenye uwajibikaji, zinazosimamia haki kwa usawa na kuweka mazingira bora ya uwekezaji na maendeleo endelevu.
Tukio hilo linaendelea kuonesha dhamira ya Serikali ya kuthamini viongozi na taasisi zinazochangia katika kuimarisha utawala wa sheria, kukuza uwajibikaji na kuhakikisha sekta ya sheria inakuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya Taifa.
Tags
Balozi Dkt.Batilda Buriani
Habari
Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
