Utekelezaji wa DIRA 2050 unahitaji uungwaji mkono wa wadau mbalimbali-Waziri wa Fedha

LONDON-Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) amesema kuwa,utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayotarajiwa kugharimu dola za Marekani trilioni 1 katika kipindi cha miaka 25 ijayo, unahitaji uungwaji mkono wa wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi kupitia uwekezaji wa kimkakati.
Mheshimiwa Balozi Omar alisema hayo jijini London nchini Uingereza, wakati wa Mkutano wa kimkakati na wawekezaji kutoka ndani na nje ya Uingereza uliofanyika katika jengo la Soko la Hisa la London (London Stock Exchange), ukiwa sehemu ya jitihada za Serikali za kuvutia mitaji ya kimataifa kwa ajili ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2050.

Alisema kuwa asilimia 70 ya mtaji unaohitajika kutekeleza Dira hiyo unatarajiwa kutoka sekta binafsi, huku asilimia 30 iliyobaki ikitarajiwa kutolewa na Serikali kupitia bajeti na mashirika yake ya umma.

Aliwashawishi wawekezaji hao kutumia fursa ya uwepo wa soko la uhakika, mazingira bora ya ufanyaji biashara, sera za kikodi zinazotabirika na vivutio vya uwekezaji, kushiriana na Serikali katika ujenzi wa uchumi wa Taifa.
“Tunatekeleza miradi ya kimkakati ambayo tunawaalika kushirikiana nasi ikiwemo Reli ya Kisasa ya SGR, upanuzi na uzalishaji wa umeme, bandari, uongezaji thamani ya bidhaa mbalimbali ikiwemo kilimo, ujenzi wa viwanja vya ndege, na madini muhimu,” alisema Mhe. Balozi Omar.

Aidha, Mhe. Balozi Omar aliwaeleza wawekezaji hao hatua kubwa zilizopigwa na Serikali kiuchumi na kijamii licha ya changamoto za kimataifa kama janga la UVIKO-19, vita ya Urusi na Ukraine na misukosuko ya kibiashara duniani, ambapo alisema uchumi wa Tanzania umeendelea kukua, ukiongezeka kwa asilimia 5.5 mwaka 2024, asilimia 5.9 mwaka 2025, na unatarajiwa kukua kwa asilimia 6.3 mwaka 2026.
Alisisitiza pia kuwa uhimilivu wa deni la Serikali unaendelea kuwa msingi wa mkakati wa fedha wa Tanzania, akitaja tathmini ya hivi karibuni ya Oktoba 2025 iliyoainisha hatari ya madeni kuwa "wastani," pamoja na ukadiriaji wa uwezo wa kukopa na kulipa madeni kutoka Taasisi za Kimataifa zinazotathimini uwezo wa nchi kukopa katika masoko ya kimataifa za Moody's, iliyoipa Tanzania alama (B1) na Fitch iliyotoa alama (B+), zote zikiwa na mtazamo thabiti.

Akizungumza katika Mkutano huo, Mkurugenzi wa Kanda ya Kusini mwa Afrika wa Shirika la Kimataifa la Internation Finance (IFC) lililoko chini ya Benki ya Dunia, Bi. Mary Porter Peschika, alisema kuwa Tanzania ni mshirika muhimu wa Taasisi hiyo na kwamba itaendelea kushirikiana nayo kwa kuiwezesha sekta binafsi pamoja na masoko ya mitaji ya ndani, kuchangia utekelezaji wa Dira 2050.
Alisema kuwa ufadhili wa IFC nchini Tanzania ulifikia zaidi ya dola bilioni 1.6 mwaka jana pekee, rekodi kubwa zaidi kuwahi kutolewa, huku akitaja fursa za ziada za uwekezaji kuwa ziko katika sekta ya nishati inayohitaji uwekezaji wa zaidi ya dola bilioni 4, kilimo, uzalishaji viwandani, afya na masoko ya mitaji ya ndani.

Mkutano huo uliwashirikisha maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Fedha, Kituo cha Uwekezaji Tanzania, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, Benki ya NMB, Benki ya Dunia, IFC, Soko la Hisa la London, Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza (FCDO) na wawekezaji mbalimbali wa taasisi za kimataifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here