NA MUNIR SHEMWETA
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo amewatahadharisha viongozi wa vijiji nchini kuacha kujihusisha moja kwa moja na uuzaji wa ardhi bila kufuata taratibu za kisheria, akisema tabia hiyo imekuwa chanzo kikubwa cha migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini.


Dkt.Akwilapo ametoa onyo hilo Julai 6, 2026 wilayani Misungwi mkoani Mwanza wakati wa hafla ya kukabidhi hati 668 za hakimiliki za kimila kwa wananchi wa vijiji vya Ndinga na Lubuga. Alisisitiza kuwa viongozi wa vijiji, wakiwemo wenyeviti, ni wasimamizi wa ardhi na si wauzaji, hivyo maamuzi ya kuuza ardhi ya kijiji yanapaswa kufanywa kwa kufuata sheria kupitia mikutano ya vijiji na kupata ridhaa ya halmashauri husika.
"Mnapotaka kuuza ardhi kwa watu lazima kijiji kupitia mikutano ya kijiji na halmashauri kikubaliane na hilo. Asije akawa mwenyekiti anaingia kwenye makubaliano peke yake. Tunapiga vita suala hilo kwa sababu limetuingiza kwenye matatizo mengi katika maeneo mbalimbali," alisema Dkt. Akwilapo, akibainisha kuwa kauli hiyo inawahusu viongozi wa vijiji kote nchini na si Misungwi pekee.
Waziri huyo pia alisisitiza kuwa Serikali haitavumilia ubaguzi wa aina yoyote katika umiliki wa ardhi, ikiwemo ubaguzi wa kijinsia, kikabila au kwa misingi mingine. Alieleza kuwa sera na sheria za ardhi zinatambua haki sawa kwa wananchi wote kumiliki ardhi, huku wataalamu wa sekta hiyo wakitakiwa kuendelea kuzisimamia ipasavyo ili kuhakikisha haki inatendeka kwa kila Mtanzania.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Bi. Johari Simizi alisema wilaya hiyo kwa sasa ndiyo eneo linalopokea kasi kubwa ya ukuaji wa makazi kutoka maeneo mengine ya Mkoa wa Mwanza, hali inayohitaji upangaji bora wa matumizi ya ardhi.
Alisema wananchi wa Misungwi wanahitaji mji uliopangwa vizuri kupitia umilikishwaji rasmi wa ardhi ili kuondoa makazi holela na kuifanya wilaya hiyo kuwa na mwonekano unaovutia.
Naye Mbunge wa Jimbo la Misungwi, Mhe. Silvery Salvatory aliitaka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuongeza elimu kwa wananchi kuhusu matumizi na umuhimu wa nyaraka za umiliki wa ardhi, akisema baadhi ya wanufaika wa hati bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu haki na wajibu unaoambatana na nyaraka hizo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Mwanza, Bw. Wilson Luge aliwapongeza wananchi wa Misungwi kwa mwitikio mkubwa wa kushiriki zoezi la urasimishaji wa ardhi, akisema hatua hiyo imeifanya wilaya hiyo kuwa mfano wa kuigwa na maeneo mengine katika juhudi za kupunguza migogoro ya ardhi kupitia upimaji na utoaji wa hati za umiliki.
Kwa niaba ya wanufaika, Bw. Shije Mashaka aliishukuru Serikali kwa kuwawezesha wananchi kumiliki ardhi kwa hati za hakimiliki za kimila, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuondoa migogoro ya mipaka iliyokuwa ikiwasumbua kwa muda mrefu.
Katika utekelezaji wa mradi wa upangaji na upimaji ardhi, Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi mkoa wa Mwanza iliipa kampuni ya GMS Geo Tech Consultancy Co. Ltd kazi ya kupima vijiji vya Ndinga na Lubuga, ambapo jumla ya hati 668 zilitolewa kwa wananchi katika awamu ya kwanza ya mradi huo.

