Wamiliki wa vibanda umiza,maduka ya kurudufu CD watakiwa kulinda maadili ya watoto

NA DIRAMAKINI

JESHI la Polisi limewakumbusha wamiliki wa vibanda umiza na maduka ya kurudufu CD na filamu katika Kata ya Mlowo Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe kuzingatia sheria na maadili kwa kutowaruhusu watoto kuingia katika maeneo hayo hususan nyakati za usiku au wakati wa kuonesha maudhui yasiyowafaa watoto.
Wito huo umetolewa Julai 14,2026 na Staff Sajenti wa Polisi Upendo Silomba wakati akizungumza na wafanyabiashara wa mji mdogo wa Mlowo kwa nyakati tofauti kuhusu kuimarisha ulinzi wa watoto na kudhibiti vitendo vinavyoweza kuhatarisha maadili yao.

Sajenti Silomba amewataka wamiliki wa vibanda umiza na maduka ya kurudufu CD na filamu kuhakikisha hawawaruhusu watoto kushuhudia maudhui yenye ukatili, matumizi ya dawa za kulevya,vitendo vya uhalifu au maudhui mengine yasiyolingana na umri wao.

Amesema,maudhui hayo yanaweza kuchangia mmomonyoko wa maadili kwa watoto na vijana, pamoja na kuongeza uwezekano wa kuiga tabia hatarishi zinazoweza kuathiri ukuaji wao na usalama wa jamii kwa ujumla.

Mbali na hilo,amewakumbusha wafanyabiashara hao kutoruhusu wala kuendesha michezo ya kubahatisha inayowashirikisha watoto, akisisitiza kuwa vitendo hivyo vinakiuka sheria na vinaweza kuwaathiri watoto kielimu, kimaadili na kijamii.

Sajenti Silomba ameeleza kuwa,wazazi, walezi, wafanyabiashara na jamii kwa ujumla wana wajibu wa kushirikiana katika kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira salama yanayowajengea maadili mema na kuwaepusha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha mustakabali wao.

Aidha,amewataka wamiliki wa biashara hizo kuzingatia kikamilifu sheria na kanuni zinazosimamia uendeshaji wa shughuli zao, huku akionya kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kukiuka taratibu zilizowekwa.

Amesisitiza kuwa,ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi, wafanyabiashara na wananchi ni muhimu katika kuimarisha ulinzi wa watoto, kupambana na mmomonyoko wa maadili na kujenga jamii yenye maadili mema na mazingira salama kwa ukuaji wa watoto na vijana.

Elimu hiyo ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za Jeshi la Polisi za kuongeza uelewa wa jamii kuhusu wajibu wa kila mmoja katika kulinda haki na ustawi wa watoto pamoja na kuzuia vitendo vinavyoweza kuhatarisha maendeleo yao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here