NA DIRAMAKINI
SERIKALI ya Uturuki imetangaza rasmi orodha ya nchi za Afrika ambazo raia wake watastahili kuomba Visa ya Kielektroniki (eVisa) kwa mwaka 2026, huku nchi tisa pekee kutoka barani humo zikijumuishwa katika utaratibu huo unaorahisisha upatikanaji wa vibali vya kuingia nchini humo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa, nchi zilizoorodheshwa ni Algeria, Cape Verde, Misri, Guinea ya Ikweta, Libya, Mauritius, Namibia, Senegal na Afrika Kusini.
Raia wa nchi nyingine zote za Afrika ikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na nyinginezo, wataendelea kuhitajika kuwasilisha maombi ya visa kupitia ubalozi au ofisi za ubalozi mdogo wa Uturuki kabla ya kusafiri.
Mfumo wa eVisa wa Uturuki unawawezesha waombaji wanaostahili kukamilisha mchakato mzima wa maombi ya visa kwa njia ya mtandao, bila kulazimika kufika katika ubalozi au ofisi za kidiplomasia.
Mfumo huo umeendelea kuwa miongoni mwa huduma zinazorahisisha safari za kimataifa kwa wageni wanaotembelea Uturuki kwa muda mfupi.
Hata hivyo, mamlaka za Uturuki zimeeleza kuwa,kustahili kutumia mfumo wa eVisa hakumaanishi kuwa mwombaji atapewa visa moja kwa moja.
Waombaji wote wataendelea kufanyiwa tathmini kulingana na uraia wao, aina ya hati ya kusafiria waliyonayo pamoja na sababu ya safari yao.
Kwa kawaida, visa ya kielektroniki hutumika kwa safari za utalii, biashara za muda mfupi na ziara nyingine zisizohitaji ukaaji wa muda mrefu, huku ikipunguza muda na gharama zinazohusiana na taratibu za kawaida za kuomba visa kupitia balozi.
Uamuzi wa Uturuki wa kuendelea kutoa huduma ya eVisa kwa idadi ndogo ya nchi za Afrika unaonesha kuwa masharti ya uingiaji nchini humo bado yanategemea sera za uhamiaji, usalama na mahusiano ya kidiplomasia kati ya Uturuki na mataifa husika.
Kwa wasafiri kutoka nchi ambazo hazimo katika orodha hiyo, mamlaka za Uturuki zimesisitiza umuhimu wa kuwasilisha maombi ya visa mapema kupitia ubalozi au ofisi za kidiplomasia ili kuepusha usumbufu kabla ya safari.
