Wananchi wa Kitongoji cha Mwemanani waiomba Serikali kupunguza gharama za kuunganishiwa umeme,waita maafisa wa TANESCO Mkuranga

MKURANGA-Wananchi wa Kitongoji cha Mwemanani kilichopo Kijiji cha Mkokozi katika Kata ya Mwandege wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani wameiomba Serikali kuingilia kati na kuweka utaratibu wa pamoja wa uunganishaji wa umeme pamoja na kupunguza gharama za kuunganishiwa huduma hiyo, ili wananchi wengi waweze kumudu na kunufaika na huduma hiyo muhimu.
Wananchi hao wamesema mradi wa kupeleka umeme katika kitongoji chao ni matokeo ya juhudi za muda mrefu walizozifanya kwa kushirikiana na Serikali ya Kijiji.

Aidha,waliwasilisha maombi rasmi ya kupelekewa umeme Machi 11,2025 na baadaye wakayakumbushia tena Oktoba 1,2025 baada ya kutopata mrejesho, hatua iliyochangia kufanikisha utekelezaji wa mradi huo.

Hata hivyo, wameeleza kuwa licha ya kukamilika kwa miundombinu ya umeme, bado hawajapatiwa elimu rasmi kuhusu hatua zinazofuata za uunganishaji wa huduma hiyo.

Kwa mujibu wao, kikao kilichokuwa kifanyike kwa ajili ya kutoa maelekezo kiliahirishwa baada ya maofisa wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kushindwa kufika, na tangu wakati huo hakujatolewa taarifa rasmi kwa wananchi.

Aidha, wananchi wamebainisha kuwa,baadhi ya kaya zinaendelea kuunganishiwa umeme mmoja mmoja bila kuwepo utaratibu wa pamoja, jambo ambalo limeibua sintofahamu na malalamiko miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.

Kutokana na hali hiyo, wananchi wa Mwemanani wameiomba Serikali kupitia TANESCO na mamlaka nyingine husika kuweka utaratibu wa wazi wa uunganishaji wa umeme, kutoa elimu kwa wananchi wote kuhusu taratibu zinazotakiwa kufuatwa, pamoja na kutathmini upya gharama za uunganishaji.
Wamesema wakazi wengi wa kitongoji hicho ni wa kipato cha chini, hivyo wameomba gharama za kuunganishiwa umeme zipunguzwe hadi kufikia takribani Shilingi 27,000, ili kaya nyingi zaidi ziweze kumudu huduma hiyo na kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika eneo hilo.

Wananchi hao wameeleza kuwa,maombi yao yalipitishwa kupitia Serikali ya Kijiji, jambo linalowapa imani kuwa Serikali itachukua hatua stahiki kuhakikisha huduma ya umeme inapatikana kwa usawa,uwazi na kwa gharama nafuu.

Miongoni mwa wananchi walioshiriki katika juhudi za kufanikisha mradi huo ni Maulidi Hassani Mpangile ambaye ni mjumbe wa wananchi, pamoja na Fredi C. Kimaru na Baraka Buyobe, waliokuwa miongoni mwa wafuatiliaji wakuu wa mradi huo.

Wengine ni Ally A. Mlanzi, Wilson George, Almasi M. Kitafo, Sadock S. Bugigwa, William Jaekob, Bahati Nyakiera, George Thobias, Hussein H. Mkande, Lucia R. Kadege, Mahamudy Suleimani, Neema E. Mjema,

Mei Tumaini, Amina Ally, Mussa Sharify, Zena Musuda (Mama Alama), Rehema Mohamedi, Hamisi Dutiro, Zena Mashoi, Salome S. Sawa, Sophia M. Nachuma, Salma A. Iddi, Elizabeti Juma Joseph, Fatuma Mohamedi, Light J. Andrew na Upendo Samweli.

Wamesisitiza kuwa,kupatikana kwa umeme kwa gharama wanazomudu wananchi wote kutafungua fursa mpya za maendeleo, ikiwemo kukuza biashara ndogo na za kati, kuboresha huduma za elimu na afya, pamoja na kuongeza ajira na kuinua ustawi wa jamii katika Kitongoji cha Mwemanani na maeneo jirani.

Kwa pamoja wameiomba Serikali kusikiliza ombi lao ili kuhakikisha mradi huo unawanufaisha wananchi wote walioupigania tangu ulipoanzishwa.

Jitihada za kupata ufafanuzi kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani zinaendelea ili kufahamu mipango waliyonayo ya kuhakikisha wananchi hao wanapata umeme kwa haraka uweze kuwasaidia katika kuchagiza shughuli za maendeleo ndani ya eneo lao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here