Wananchi wajifunza kutambua ubora wa Madini ya Vito

DAR-Wananchi wanaotembelea banda la Tume ya Madini katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SabaSaba) wanaendelea kunufaika na elimu kuhusu matumizi ya kifaa cha Gemmological Torch, kinachotumika kutambua ubora na thamani halisi ya madini ya vito.
Akitoa elimu katika banda hilo, Mjiolojia na Mjimolojia Mwandamizi kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Mirerani, Selemani Khamisi, amesema thamani ya madini ya vito hupimwa kwa kuzingatia vigezo vinne vikuu vinavyojulikana kitaalam kama 4Cs, ambavyo ni rangi (Colour), uzito (Carat), ubora (Clarity) na umbo la ukataji (Cut).

Amesema pamoja na matumizi ya Gemmological Torch, wataalam pia hutumia vifaa vingine vya kitaalam ikiwemo Head Loupe, Table Lamp na Price Guide ya Serikali ili kufanya tathmini ya kina ya ubora wa jiwe.

Uchunguzi huo huwezesha kubaini nyufa, mipasuko, uchafu wa ndani (inclusions), pamoja na ubora na ukolezi wa rangi ya jiwe.
"Kadiri jiwe linavyokuwa na rangi ang’avu, ubora mzuri wa ndani, uzito mkubwa na ukataji mzuri, ndivyo thamani yake inavyoongezeka. Matumizi ya vifaa kama Gemmological Torch na Head Loupe hutuwezesha kubaini sifa hizo kwa usahihi,” amesema Khamisi.

Ameongeza kuwa madini ya vito yaliyovutia zaidi wananchi wanaotembelea banda la Tume ya Madini ni Tanzanite ghafi na iliyoongezwa thamani, Green Garnet, Tourmaline na Almandite Garnet, ambapo wageni wamekuwa wakipata fursa ya kujifunza sifa, ubora na thamani ya kila aina ya jiwe la vito.

Khamisi amewahimiza wananchi, wafanyabiashara wa madini na wadau wengine wa sekta ya madini kutembelea banda la Tume ya Madini ili kujifunza matumizi ya vifaa vya kisasa vya uchunguzi wa madini ya vito, vinavyosaidia kufanya tathmini sahihi ya ubora na thamani ya madini hayo kabla ya kuyauza au kuyanunua.
Amesema,elimu hiyo ni sehemu ya juhudi za Tume ya Madini za kuongeza uelewa wa umma kuhusu biashara ya madini ya vito, kuimarisha uwazi katika biashara hiyo na kuongeza thamani ya rasilimali za madini nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here