NA DIRAMAKINI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Watanzania wanahitaji kuendelea kuishi katika mazingira ya amani, usalama na utulivu badala ya vurugu na mivutano ya kisiasa, akisisitiza kuwa hali hiyo ndiyo msingi wa serikali kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake ya kutoa huduma za kijamii, kukuza uchumi na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Julai 9,2026 katika Viwanja vya Ikulu Zanzibar wakati wa hafla ya kushuhudia utiaji saini wa Tamko la Pamoja la Maridhiano ya Kisiasa kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo, tukio lililoelezwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha mshikamano wa kisiasa na ustawi wa Zanzibar.
Akihutubia viongozi wa kisiasa, serikali,dini na wageni mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo, Rais Samia amesema,maridhiano ya kisiasa hayapaswi kutafsiriwa kama ishara ya udhaifu, bali ni kielelezo cha ukomavu wa kisiasa na uwezo wa viongozi kuweka mbele maslahi ya taifa kuliko tofauti za kisiasa.
Amesema,maridhiano hayo yanafungua ukurasa mpya wa kujenga mazingira ya kuheshimiana, kushirikiana na kufanya siasa za ustaarabu zinazojengwa katika hoja na mazungumzo, badala ya chuki, migawanyiko na mivutano inayoweza kuathiri maendeleo ya wananchi.
"Watanzania wanahitaji amani, usalama na utulivu. Hayo ndiyo mazingira yanayowezesha Serikali kuendelea kuboresha huduma za kijamii, kukuza uchumi na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi,"amesema Rais Samia.
Ameongeza kuwa,migogoro ya kisiasa na siasa za chuki huchelewesha maendeleo na kupunguza kasi ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo, huku maridhiano yakijenga msingi imara wa ustawi wa jamii na maendeleo endelevu.
Rais Samia amewataka wote waliohusika katika kufanikisha maridhiano hayo kuendelea kuheshimu makubaliano yaliyofikiwa, kuendeleza mazungumzo ya wazi na kujenga imani kwa lengo la kulinda umoja wa kitaifa na kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kudumu nchini.
Akihitimisha hotuba yake, Rais Samia amesisitiza umuhimu wa kulinda mafanikio yaliyopatikana kupitia maridhiano hayo."Hekima tuliyoionesha leo ikalindwe kwa matendo mema ya kesho, na imani tuliyoijenga kwa muda mrefu isiangushwe kwa maneno au mienendo isiyo na tija,"amesema.
Kwa upande wake, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema,Tamko la Pamoja la Maridhiano kati ya CCM na ACT-Wazalendo linafungua njia ya utekelezaji wa uundaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kuimarisha amani, umoja, mshikamano na maendeleo ya Zanzibar.
Dkt.Mwinyi amesema,makubaliano hayo yanaonyesha dhamira ya kweli ya viongozi wa kisiasa kuweka mbele maslahi ya taifa na wananchi, huku akiahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha mchakato huo unatekelezwa kwa mafanikio na unachangia kuimarisha utawala bora, utulivu na maendeleo endelevu.
Naye Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman amempongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa kuendeleza mchakato wa maridhiano akieleza kuwa,hatua hiyo imefungua njia ya kupatikana kwa suluhisho la kudumu la changamoto za kisiasa zilizodumu kwa muda mrefu Zanzibar.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa na Zanzibar, akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, Marais Wastaafu wa Zanzibar Dkt. Amani Abeid Karume na Dkt. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla, viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini, viongozi wa Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, mabalozi, wawakilishi wa taasisi za kimataifa pamoja na wananchi mbalimbali.Maridhiano hayo yanatajwa kuwa hatua muhimu katika kuendeleza utamaduni wa mazungumzo na kujenga mazingira ya kisiasa yenye utulivu, jambo linalotarajiwa kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi pamoja na kudumisha amani ya kudumu Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.








