ACCRA-Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo (Mb) ameshiriki Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika ngazi ya Mawaziri kuhusu masuala ya Afya (Extraordinary Summit on Health).
Mkutano huo ambao utahudhuriwa pia na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, unafanyika jijini Accra nchini Ghana tarehe 21 Julai, 2026 kwa ngazi ya Mawaziri na tarehe 22 Julai, 2026 kwa ngazi ya Wakuu wa nchi na Serikali.
Mkutano huo wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika unatokana na Azimio la Umoja wa Afrika Na. 908 kuhusu kuitishwa Mkutano wa Dharura ili kujadili namna ya kutokomeza ugonjwa wa UKIMWI ifikapo mwaka 2030, Kudhibiti vifo vya Mama na Mtoto, magonjwa yanayoambukizwa na yasiyo ambukizwa na kuimarisha Mifumo ya Afya barani Afrika ifikapo mwaka 2030, pia Mkutano huo utapitisha Azimio la kutekeleza Mpango Kazi wa Umoja wa Afrika.






