TANGA-Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) ameongoza kikao cha maandalizi ya ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Tanga ambapo anatarajiwa kutembelea shughuli mbalimbali ikiwemo miradi ya maendeleo mkoani humo.
Katika kikao hicho alipokea taarifa ya Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ambaye pia ni Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA Leonard Mkude, Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Bw. Mcha Hassan Mcha, baadhi ya wakurugenzi, makamishna kutoka Wizara ya Fedha na Wataalamu wengine kutoka taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo Mamlaka ya Bandari Tanzania, mkoa wa Tanga.
Akizungumza katika kikao hicho Mhe. Balozi Omar alisema ziara hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano na mawasiliano ya karibu kati ya Serikali na wananchi ili kuwawezesha kuelewa namna mipango ya maendeleo na bajeti ya Serikali inavyogusa maisha yao.
"Lengo la ziara hii pia ni kutembelea na kuangalia fursa za kiuchumi na kijamii zinazopatikana katika mkoa wa Tanga, ikiwemo Bandari, Viwanda, Biashara mipakani na huduma za kijamii na pia kuangalia namna bajeti kuu ya Serikali iliyopitishwa hivi karibuni inavyoweza kuwanufaisha wakazi wa mkoa huu ikiwemo kukuza ajira kupitia miradi hiyo,”amesema Mhe. Balozi Omar.
Aidha alisema kuwa ziara hiyo itatoa fursa ya kujadili utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa Tanga, ikiwemo maendeleo ya Bandari ya Tanga, ujenzi wa barabara ya Tanga-Pangani-Bagamoyo kupitia Saadani, mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), Uwekezaji katika sekta za elimu, afya, viwanda, Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), na namna Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inavyoweza kufikia malengo ya kukusanya zaidi ya shilingi trilioni 41 kwa ajili ya kutekeleza bajeti ya Serikali.





