DAR-Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) ameongoza mamia ya waombolezaji katika maziko ya mama mzazi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, marehemu Bi. Hajjat Nayma Said El-Maamry, yaliyofanyika katika Makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam.
Mazishi hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, watumishi wa Wizara ya Fedha, ndugu, jamaa na marafiki waliojitokeza kutoa heshima zao za mwisho kwa marehemu na kuifariji familia.
Miongoni mwa viongozi wa Wizara ya Fedha walioshiriki maziko hayo ni Naibu Mawaziri wa Fedha, Mhe. Mshamu Ali Munde na Mhe. Laurent Luswetura. Wengine ni Naibu Katibu Mkuu, Bw. Elijah Mwandumbya, Naibu Katibu Mkuu, Bw. Nsubili Joshua, pamoja na Kaimu Naibu Katibu Mkuu ambaye pia ni Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje, Bw. Rished Bade.
Aidha, Wakuu wa Idara, Vitengo na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha pia walishiriki katika shughuli hiyo ya kuaga mwili wa marehemu na maziko yake. Marehemu Hajjat Nayma Said El-Maamry alifariki dunia Julai 17, 2026, jijini Dar es Salaam.
Wizara ya Fedha, inatoa pole kwa Dkt. Natu El-Maamry Mwamba na familia yote na kuwaombea Mwenyezi Mungu awape nguvu, faraja na ustahimilivu katika kipindi hiki cha majonzi.









