Waziri wa Fedha atoa rai kwa wasimamizi na viongozi wa Kituo cha Michezo cha Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) cha Mnyanjani

TANGA-Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, ametoa rai kwa wasimamizi na viongozi wa Kituo cha Michezo cha Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) cha Mnyanjani, kilichoko mkoani Tanga, kuhakikisha kuwa, pamoja na kukuza vipaji vya soka, wanajenga kizazi cha vijana wenye maadili, nidhamu na elimu, ili kuwaandaa kuwa wanamichezo mahiri wa sasa na baadae.
Balozi Omar alitoa rai hiyo alipotembelea kituo hicho na kufanya mazungumzo na Meneja wa Oparesheni wa Kituo, Kassim Haji, pamoja na Kocha wa Vipaji kutoka Uingereza, Edwanly Monnely, ambapo alipata fursa ya kujionea maendeleo ya programu za ukuzaji vipaji vinavyoendeshwa na kituo hicho.

Alisema kuwa mataifa mengi duniani yamefanikiwa kuibua vipaji vya hali ya juu kupitia uwekezaji mkubwa katika michezo, lakini baadhi ya wanamichezo walishindwa kufikia mafanikio yaliyokusudiwa kutokana na kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya na vitendo vingine vinavyokwenda kinyume na maadili ya michezo.

"Ni muhimu kuwalea vijana katika misingi ya maadili sambamba na kuwanoa kimichezo ili waweze kufanikiwa ndani na nje ya uwanja," alisema Balozi Omar.
Alisisitiza kuwa nidhamu na maadili ni nguzo muhimu katika kumjenga mwanamichezo bora, akieleza kuwa mafanikio ya kweli katika soka hayaishii uwanjani pekee, bali yanahitaji pia tabia njema na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi katika maisha.

Aidha, Balozi Omar alisisitiza umuhimu wa vijana wanaopatiwa mafunzo ya soka kuendelea na elimu ya darasani, akieleza kuwa elimu huongeza upeo wa fikra, huimarisha nidhamu na huwapa uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali hata baada ya kumaliza maisha yao ya uchezaji.

Alibainisha kuwa,mchanganyiko wa elimu, maadili na mafunzo bora ya michezo ndiyo msingi wa kuzalisha wachezaji wenye mafanikio endelevu watakaoweza kupeperusha vyema Bendera ya Tanzania katika mashindano ya kimataifa.
Kwa upande wake, Meneja wa Oparesheni wa Kituo hicho, Kassim Haji, na Kocha wa kuendeleza alimshukuru Balozi Omar kwa kutembelea kituo hicho na kupata nafasi ya kujionea mazingira halisi ya mafunzo pamoja na maendeleo ya vijana wanaolelewa kupitia programu za ukuzaji vipaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here