Waziri wa Fedha atoa wito kwa wanafunzi wote nchini

TANGA-Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) amewataka wanafunzi nchini kutumia ipasavyo fursa ya elimu wanayoipata kwa kujikita katika masomo yao, akisisitiza kuwa elimu ndiyo msingi wa mafanikio ya mtu binafsi na maendeleo ya taifa.
Rai hiyo aliitoa wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Bweni la wanafunzi wavulana wa kidato cha tano na cha sita katika Shule ya Sekondari ya Usagara mkoani Tanga.

Mhe. Balozi Omar alisema jukumu kuu la mwanafunzi ni kusoma kwa bidii na kujiandaa kwa maisha ya baadaye.

"Jukumu la wanafunzi ni kusoma, huu ndiyo muda wenu wa kujifunza na kujiandaa kwa maisha yenu ya baadaye. Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia, walimu wanatoa maarifa na wazazi wanatimiza wajibu wao wa kuwalea na kuwahudumia. Kilichobaki kwa wanafunzi ni kufanya bidii katika masomo yenu", alisema Mhe. Balozi Omar.

Alibainisha kuwa Serikali inaendelea kuwekeza katika sekta ya elimu kwa kuboresha miundombinu ya shule, ikiwemo ujenzi wa mabweni, madarasa na huduma nyingine muhimu zinazochochea ufaulu wa wanafunzi.

Alisema mabweni yana mchango mkubwa katika kuongeza muda wa kujifunza, kuimarisha nidhamu na kuboresha matokeo ya mitihani, ndiyo maana Serikali imeendelea kuyapa kipaumbele katika shule mbalimbali nchini.
Mhe. Omar aliwapongeza walimu wa Shule ya Sekondari ya Usagara kwa kazi nzuri ya kuwalea na kuwafundisha wanafunzi, akiwataka kuendelea kujituma ili kuongeza kiwango cha ufaulu na kuandaa wahitimu wenye maarifa na maadili mema.

Aidha, alisema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kuboresha sekta ya elimu kupitia uwekezaji wa miundombinu ya kisasa, hatua inayolenga kuhakikisha kila mwanafunzi anapata mazingira bora ya kujifunzia na kutimiza ndoto zake.

Alieleza kuwa kukamilika kwa bweni hilo kutawawezesha wanafunzi wengi zaidi kuishi shuleni, kupunguza muda wanaotumia kutembea kwenda na kurudi nyumbani na kuongeza muda wa kujisomea, jambo litakalosaidia kuinua zaidi kiwango cha ufaulu wa shule hiyo kongwe.

Katika kuunga mkono jitihada hizo, Mhe. Omar aliahidi Serikali kutoa shilingi milioni 37 kwa ajili ya ununuzi wa vitanda ili bweni hilo lianze kutumika hususani kwenye sakafu ya chini ambayo imekamilika.
Bweni hilo la ghorofa tatu linajengwa kwa ushirikiano kati ya Serikali Kuu na Halmashauri ya Jiji la Tanga na litakuwa na uwezo wa kuhudumia wanafunzi 240 wa kidato cha tano na sita.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Usagara, Bw. Alex Ilumo, alisema jitihada za kuendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia zimechangia kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu wa wanafunzi wa shule hiyo kutoka asilimia 91.9 hadi asilimia 99.

Alisema mradi huo, ambao hadi sasa una thamani ya shilingi milioni 424, umefikia hatua ya umaliziaji, ambapo sakafu ya chini imekamilika kwa asilimia 90 baada ya kutumika shilingi milioni 359.1, ambapo kwa ujumla mradi unatarajiwa kugharimu takribani shilingi bilioni 1.07.
Bw.Ilumo aliongeza kuwa Halmashauri ya Jiji la Tanga imetenga shilingi milioni 647 kutoka katika mapato yake ya ndani kwa mwaka huu wa fedha ili kuhakikisha ujenzi wa bweni hilo unakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wanafunzi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here