TANGA-Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ametoa wito kwa wananchi wenye mahitaji maalumu kuchangamkia fursa za kuomba zabuni za Serikali kupitia Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST), kwa kuwa Serikali imetenga asilimia 30 ya zabuni za umma kwa makundi maalum ili kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi na kuchochea maendeleo jumuishi nchini.

Amesema hayo wakati wa Hafla ya Kugawa Miguu Bandia kwa watu wenye mahitaji maalumu, iliyoratibiwa na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Tanga Mhe. Mwanaisha Ulenge, pamoja na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Ng’arisha Maisha, iliyofanyika katika Ukumbi wa Regal Naivera, jijini Tanga.
Mhe. Balozi Omar alisema Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki kupitia Sheria na Kanuni za Ununuzi wa Umma zinazolenga kuwawezesha wazawa pamoja na makundi maalum kushiriki kikamilifu katika zabuni za Serikali, akibainisha kuwa zabuni zenye thamani ya hadi shilingi bilioni 50 hutangazwa ndani ya nchi ili kuwapa kipaumbele wazawa, huku hata zabuni zinazotangazwa kimataifa zikiendelea kutenga asilimia 30 kwa makundi hayo.
Alisisitiza kuwa wananchi wenye mahitaji maalumu wanapaswa kuutumia kikamilifu Mfumo wa NeST kuomba zabuni za Serikali katika maeneo mbalimbali ikiwemo usambazaji wa bidhaa, utoaji wa huduma na kazi za ujenzi, badala ya kuziacha fursa hizo zipite, akieleza kuwa Serikali imeweka mifumo na sera zinazolenga kuwainua kiuchumi na kuongeza ushiriki wao katika maendeleo ya taifa.
"Nawahimiza vijana, wanawake na makundi mengine maalum kuendelea kujijengea uwezo na kushiriki katika mafunzo mbalimbali yanayotolewa kuhusu fursa za zabuni za umma ili waweze kushindana na kunufaika na nafasi hizo,”alisema Mhe. Balozi Omar.
Akizungumzia msaada wa miguu bandia uliotolewa, Mhe. Balozi Omar amesema vifaa hivyo vitawawezesha walengwa kurejea katika shughuli za uzalishaji na kujitegemea kiuchumi, huku akiwasihi kuvitunza na kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ili viwe na manufaa ya kudumu.
Mhe. Balozi Omar alimpongeza Mhe. Mwanaisha Ulenge pamoja na wadau wote waliofanikisha zoezi hilo, akieleza kuwa jitihada za kuwainua wananchi wenye mahitaji maalumu zinapaswa kuungwa mkono na kila mmoja kwa kuwa ni sehemu Muhimu ya maendeleo jumuishi ya Taifa.
“Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kupeleka huduma za maendeleo na kuhakikisha makundi yote ya wananchi yanapata fursa sawa za kushiriki katika shughuli za kiuchumi na maendeleo ya nchi,” alisema Mhe. Balozi Omar.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Tanga Mhe. Mhandisi Mwanaisha Ulenge, aliipongeza Serikali kwa uamuzi wake wa kuifanyia tathmini Sheria ya Ununuzi wa Umma ibara 410 ya mwaka 2006, na marekebisho yake ambayo mpaka sasa ina miongo miwili ambayo imetoa fursa kwa makundi mbalimbali hasa vijana, wanawake na makundi maalum.
Mhe. Mhandisi Ulenge alisema kuwa,kwa mujibu wa tafiti iliyofanywa na Trade Mark East Afrika wakishirkiana na Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC) mwaka 2021 ushiriki wa Wanawake ulikuwa 2% tu na makundi mengine ni chini ya hapo, hivyo anaipongeza Serikali kwa kuamua kuifanyia tathmini utekelezaji wa sheria hiyo.














