Wiki ya Elimu,Ujuzi na Ubunifu 2026 kulenga kuchochea utekelezaji wa Dira 2050

NA GODFREY NNKO

SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia imetangaza kuwa,Maadhimisho ya Wiki ya Taifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu mwaka 2026 yatafanyika kuanzia Agosti 15 hadi 20 katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara mkoani Tanga, yakilenga kuonesha namna elimu, ujuzi,sayansi,teknolojia na ubunifu vinavyoweza kuwa injini ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Hayo yameelezwa leo Julai 30,2026 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Profesa Mkenda amesema, maadhimisho hayo yatakuwa jukwaa la kuwakutanisha wadau mbalimbali kwa ajili ya kuonesha mafanikio, kubadilishana uzoefu na kujadili fursa za kutumia maarifa na teknolojia katika kukuza maendeleo ya Taifa.

Amesema,pia maadhimisho hayo yatawakutanisha wizara na taasisi mbalimbali za Serikali, taasisi za elimu ya juu na utafiti, vyuo vya ufundi na ualimu, shule, wabunifu, watafiti, kampuni za teknolojia, sekta binafsi na wadau wa maendeleo.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Elimu, Ujuzi na Ubunifu: Njia ya Kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050”, ambayo kwa mujibu wa Waziri Mkenda inalenga kuhamasisha matumizi ya maarifa, ujuzi na teknolojia katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Profesa Mkenda amesema,maadhimisho hayo yatakuwa na maonesho ya teknolojia, bidhaa na bunifu mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, hatua inayolenga kutoa fursa kwa wananchi kujionea kwa vitendo maendeleo yanayofanyika katika maeneo ya sayansi, teknolojia na ubunifu.

Amesema, pia kutakuwa na Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi,Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU), mashindano ya ujuzi kwa wanafunzi wa vyuo vya ufundi, makongamano ya kitaaluma, warsha pamoja na huduma zinazohusu hakimiliki na ulinzi wa bunifu.

Kwa mtazamo wa Serikali, shughuli hizo zitatoa nafasi kwa wabunifu kuonesha bidhaa zao, kupata fursa za kujenga mitandao ya kibiashara na kitaalamu na kuunganishwa na wadau wanaoweza kusaidia bunifu zao kufikia hatua ya uzalishaji na matumizi ya kibiashara.

Waziri Mkenda amesema,Serikali imeanza kuona matokeo ya juhudi za kuhamasisha ubunifu kupitia mashindano ya MAKISATU, akibainisha kuwa baadhi ya bunifu zilizoibuliwa kupitia mashindano hayo tayari zimeingia sokoni na kuanza kuwa chanzo cha kipato kwa wabunifu wake.
Miongoni mwa bunifu hizo ni mashine ya kukamua mafuta ya parachichi (Avomero), mabegi ya shule yenye mfumo wa sola, vifaa vya kuwasaidia wanafunzi wenye ulemavu, teknolojia za kuchakata vyakula vya mifugo pamoja na mita janja za maji.

Profesa Mkenda amesema, hali hiyo inathibitisha kuwa ubunifu wa Watanzania hauishii katika maonesho, bali unaweza kubadilishwa kuwa bidhaa na huduma zinazotatua changamoto za jamii na kuchangia ukuaji wa uchumi.

“Wapo wanaodhani bunifu zinaishia kwenye maonesho pekee, lakini ukweli ni kwamba zipo nyingi ambazo tayari zimeingia sokoni na wabunifu wake wanafanya biashara. Serikali inaendelea kuwawezesha wabunifu kuhakikisha teknolojia zao zinawanufaisha wananchi na uchumi wa Taifa,”amesema Profesa Mkenda.

Aidha, Waziri Mkenda amesema Serikali inaendelea kusimamia takribani bunifu 70 zilizo katika hatua mbalimbali za maendeleo, huku ikiimarisha mazingira ya kuzifikisha sokoni kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali pamoja na sekta binafsi.
Hatua hiyo inalenga kuondoa changamoto ya bunifu nyingi kubaki katika hatua ya wazo au mfano wa bidhaa bila kufikia hatua ya uzalishaji wa kibiashara.

Kwa mujibu wa Waziri, Serikali inaona umuhimu wa kuweka mazingira yatakayomwezesha mbunifu kutoka katika hatua ya kubuni, kufanya majaribio, kupata ulinzi wa haki miliki na hatimaye kuzalisha bidhaa au huduma inayoweza kutumika na jamii.

Vilevile, Profesa Mkenda amesema Wizara imeanzisha Madawati ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu katika halmashauri mbalimbali nchini kwa lengo la kurahisisha utambuzi wa wabunifu na kuwapatia msaada unaohitajika.

Amesema,hadi sasa halmashauri 90 tayari zimeanzisha madawati hayo, huku Serikali ikiwa na lengo la kuhakikisha huduma hiyo inapatikana katika halmashauri zote nchini.
Madawati hayo yanatarajiwa kuwa kiungo muhimu kati ya wabunifu waliopo katika maeneo mbalimbali na taasisi zinazohusika na elimu, teknolojia, fedha, utafiti, hakimiliki na masoko.

SERIKALI YATAFUTA MITAJI NA MASOKO

Profesa Mkenda amesema Serikali pia imeendelea kutafuta njia za kuwawezesha wabunifu kupata mitaji ya kuendeleza biashara zinazotokana na teknolojia na mawazo yao.

Amesema,Serikali kwa kushirikiana na Benki ya CRDB imeweka utaratibu wa kuwawezesha wabunifu kupata mitaji, huku ikiendelea kushirikiana na Watanzania wanaoishi nje ya nchi ili kutafuta masoko, utaalamu na fursa za uwekezaji katika sekta ya sayansi na teknolojia.
Hatua hiyo inalenga kuunganisha ubunifu na fursa za kifedha na masoko, kwa kuwa changamoto kubwa inayowakabili wabunifu katika hatua za awali ni uwezo wa kubadilisha teknolojia zao kuwa bidhaa zinazoweza kuzalishwa kwa wingi na kuuzwa.

Akizungumzia changamoto zinazowakabili baadhi ya wabunifu, Waziri Mkenda amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi husika kuhakikisha bunifu zinazohitaji uthibitisho wa kitaalamu zinakamilisha taratibu zinazohitajika kwa wakati.

Hata hivyo, amesema taratibu hizo lazima zizingatie viwango vya ubora na usalama, hususan bidhaa zinazohusiana na afya ya binadamu.

Kauli hiyo inaweka mkazo katika umuhimu wa kuhakikisha kwamba juhudi za kuharakisha ubunifu kufikia soko haziathiri viwango vinavyotakiwa kwa bidhaa zinazotumika na wananchi.

Maadhimisho hayo yanatarajiwa kuwa fursa ya kuendelea kuonesha uhusiano kati ya elimu, ujuzi, teknolojia na maendeleo ya Taifa.

Katika mazingira ambayo uchumi wa dunia unazidi kutegemea maarifa na teknolojia, uwezo wa Taifa kuzalisha wataalamu, wabunifu na wajasiriamali wenye ujuzi unakuwa sehemu muhimu ya ushindani wa kiuchumi.

Kwa Tanzania, kuwekeza katika elimu, ujuzi na ubunifu kunaweza kusaidia kuongeza uzalishaji, kutengeneza ajira, kuongeza thamani ya bidhaa za ndani, kupunguza utegemezi wa teknolojia kutoka nje na kutoa suluhisho kwa changamoto zinazolikabili Taifa.

Kwa msingi huo, kaulimbiu ya mwaka huu inasisitiza kwamba utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 hauwezi kutenganishwa na uwezo wa Watanzania kuzalisha na kutumia maarifa katika kutatua changamoto za maendeleo.

WADAU WAHIMIZWA KUSHIRIKI

Waziri Mkenda ametoa wito kwa taasisi za umma na binafsi, watafiti, wabunifu, wanafunzi na wananchi kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Wiki ya Taifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu 2026.

Amesema,ushiriki huo utatoa fursa kwa wananchi kujionea teknolojia na bunifu zinazotengenezwa na Watanzania, kuelewa fursa zinazopatikana na kujifunza namna elimu, ujuzi na ubunifu vinavyoweza kutumika katika kujenga uchumi wenye tija.
Maadhimisho hayo ya siku sita yanatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kuunganisha elimu, utafiti, teknolojia, ubunifu na biashara, huku yakitoa msukumo mpya katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi unaotegemea zaidi maarifa, ujuzi na teknolojia.

Kwa kufanyika katika mkoani Tanga, tukio hilo pia linatoa nafasi ya kupeleka mjadala wa sayansi, teknolojia na ubunifu nje ya Dar es Salaam na kuwawezesha wananchi wa maeneo mbalimbali kushiriki katika ajenda ya Taifa ya maendeleo ya maarifa na ubunifu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here