DC Kyobya mgeni rasmi tukio la kihistoria la Hike for a Girl Child huko Udzungwa

KILOMBERO-Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Msomi Dkt. Dunstan Kyobya anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi kwenye tukio la kihistoria la Matembezi ya Vilimani ili kupaza Sauti kwa Ajili ya Mtoto wa Kike, "Hike for A Girl Child".
Tukio hilo lenye lengo la kuvunja ukimya na unyanyapaa masuala ya Hedhi Salama kwa Watoto wa Kike, litafanyika tarehe 2 Agosti 2026, katika Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa, Wilaya ya Kilombero, Mkoa wa Morogoro.

Kwa mujibu wa Waratibu wa kampeni hiyo kutoka The Brighter Binti Foundation, Dkt. Kyobya anatarajiwa kuzindua daraja la Utalii katika njia ya Sonjo Route tayari kwa matembezi ya vilimani.

"Agosti 2, saa 1:00 Asubuhi, Mkuu wa Wilaya Dkt. Kyobya atazindua rasmi daraja la Utalii, kisha kufanya 'Hike' njia ya maporomoko ya maji ya Sanje ambapo washiriki wote tutajumuika," wamesema waratibu hao.

Mchana, matukio mengine yatafanyika Shule ya Sekondari Sanje ambapo kutakuwa na shughuli mbalimbali zikiwemo: Mawasilisho mafupi juu ya Mwongozo wa Hedhi Salama, Elimu ya Malezi ya Familia, Afya ya Akili na Saikolojia.

Pia kutakuwa na Clinic ya Hedhi Salama kwa Jamii, Wanafunzi na Walimu, Maonesho ya bidhaa za Hedhi, Hotuba fupi ya Dkt. Kyobya kwa Wananchi, Wanafunzi na Wadau, sambamba na Utoaji wa Taulo za Hedhi kwa Shule ya Sekondari Sanje na zile za karibu kuzunguka Hifadhi ya Udzungwa.

The Brighter Binti Foundation wanasema wanaamini mabadiliko huanza na Jamii, hivyo matembezi hayo ya vilimani yataongeza umuhimu wa jamii kwa ujumla katika kuelewa na kuondoa unyanyapaa wa hedhi hapa nchini.

"Mabadiliko huanza pale jamii inapopata uelewaji sahihi na kuondoa unyanyapaa wa hedhi. Tunapanda mlima huu sio kwa raha tu. Tunapanda kwa ajili ya Mtoto wa Kike."

The Brighter Binti Foundation imewashukuru wadau wote wakiwemo: *Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Halimashauri ya Wilaya ya Kilombero, Hifadhi ya Taifa ya Udzungwa - TANAPA, TASACI, RTU, Wizara ya Afya, SAFEPAD, She Foundation Tanzania, ICON, FOCAYO, Next Fox Adventures, ARQ, PEPAIN, ToneHai, ONE DRAIN, SAWA* na wadau wengine.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here