NA DIRAMAKINI
YOUNG Africans Sports Club (Yanga SC) imemtambulisha rasmi kocha raia wa Afrika Kusini, Manqoba Mngqithi kuwa Kocha Mkuu mpya wa timu hiyo kuelekea msimu wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara 2026/2027, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha kikosi kwa ajili ya mashindano ya ndani na kimataifa.
Mngqithi anajiunga na mabingwa hao wa Tanzania akiwa na uzoefu mkubwa wa kufundisha soka la kiwango cha juu barani Afrika, hususan katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL), ambako amejijengea sifa kutokana na mafanikio aliyoyapata akiwa na vilabu mbalimbali.
Kocha huyo aliitumikia kwa zaidi ya muongo mmoja klabu ya Mamelodi Sundowns, kuanzia mwaka 2013 hadi 2024, akifanya kazi katika nafasi tofauti za benchi la ufundi.
Katika kipindi hicho alihudumu kama Kocha Msaidizi kuanzia mwaka 2013 hadi 2020, baadaye akapandishwa kuwa Kocha Mkuu Msaidizi mwaka 2022, kabla ya kupewa jukumu la kuinoa timu kama Kocha Mkuu mwaka 2024.
Akiwa Mamelodi Sundowns, Mngqithi alishiriki katika mafanikio makubwa ya klabu hiyo ikiwemo kutwaa mataji mbalimbali ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini na kufanya vizuri katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, jambo lililomjengea heshima kama mmoja wa makocha wenye uzoefu mkubwa katika soka la bara la Afrika.
Kabla ya kutua Jangwani, Mngqithi alikuwa Kocha Mkuu wa klabu ya Golden Arrows, ambapo aliiongoza timu hiyo kumaliza katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa mwisho wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini msimu uliopita.
Ujio wa Mngqithi unatarajiwa kuongeza nguvu katika benchi la ufundi la Yanga huku mashabiki wa klabu hiyo wakitarajia kuona timu ikiendeleza ubora wake katika kutetea mataji ya ndani pamoja na kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya kimataifa, hususan Ligi ya Mabingwa Afrika.
Aidha,uteuzi wa kocha huyo umetokana na uzoefu wake mkubwa, uwezo wa kuendeleza vipaji vya wachezaji na rekodi yake ya ushindani katika soka la Afrika, ukiamini atasaidia kutimiza malengo ya klabu katika msimu mpya wa 2026/2027.
