Yusuph Kileo awataka watumiaji wa intaneti na mitandao ya kijamii kuzingatia sheria kujiweka salama dhidi ya uhalifu wa kidijitali

NA DIRAMAKINI

MTAALAMU wa Masuala ya Usalama wa Mtandao na Uchunguzi wa Makosa ya Mtandao, Yusuph Kileo amewataka watumiaji wa intaneti na mitandao ya kijamii kutumia majukwaa hayo kwa kuzingatia sheria na misingi ya maadili ili kukabiliana na ongezeko la vitisho vya kidijitali.
Kileo amesema matumizi yanayowajibika ya mitandao ya kijamii ni muhimu katika kupunguza uhalifu wa kimtandao, ikiwemo uonevu wa mtandaoni,wizi wa utambulisho, utapeli, ufuatiliaji wa mtu mtandaoni, unyanyasaji pamoja na kuenea kwa matamshi ya chuki.

Amesema,watumiaji wa intaneti wanapaswa kuhakikisha kuwa vitendo vyao katika mazingira ya kidijitali vinaendana na mifumo ya sheria iliyowekwa, kwa kuwa kufanya hivyo kutasaidia kupunguza vitisho vinavyoweza kuathiri usalama, heshima, mali na haki za watu wengine.

Kwa mujibu wa Kileo, ukuaji wa kasi wa mitandao ya kijamii umeleta mapinduzi makubwa katika mawasiliano duniani kwa kuwawezesha watu kupata na kusambaza taarifa kwa urahisi, lakini pia umewapa watu wenye nia ovu fursa pana ya kutumia majukwaa hayo kutekeleza uhalifu.

Amesema,baadhi ya watu wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kufanya vitendo vya uonevu, wizi wa utambulisho, unyanyasaji, ufuatiliaji wa watu bila ridhaa na aina nyingine za makosa ya mtandao.

“Tunapaswa kuhimiza matumizi ya mtandao yanayozingatia sheria ili kupunguza vitisho vya kidijitali kama vile uonevu wa mtandaoni, wizi wa utambulisho, utapeli na kuenea kwa matamshi ya chuki,"amesema.

Kileo amesisitiza kuwa,kulinda uhuru wa kidijitali wakati huo huo kukabiliana na uhalifu wa mtandao si mambo yanayopingana, bali ni wajibu wa pamoja unaohitaji ushirikiano wa Serikali, kampuni za teknolojia na watumiaji wa mitandao.

Amesem,Serikali ina wajibu wa kuweka mifumo madhubuti ya kisheria na mipaka iliyo wazi kuhusu matumizi ya mitandao, huku kampuni za teknolojia zikitakiwa kuchukua hatua za kuimarisha usalama wa watumiaji na kupunguza matumizi mabaya ya majukwaa yao.

Kwa upande wa watumiaji, amesema kuna umuhimu wa kuimarisha uelewa wa kidijitali ili watu waweze kutambua hatari zinazoweza kujitokeza mtandaoni, kulinda taarifa zao binafsi na kutumia mitandao kwa usalama na uwajibikaji.

Kileo amesema,elimu ya kidijitali ni nyenzo muhimu katika kujenga jamii inayoweza kukabiliana na vitisho vya mtandaoni, kwa kuwa watumiaji wenye uelewa wana uwezo mkubwa wa kutambua ulaghai, kulinda akaunti zao na kuepuka kushiriki katika vitendo vinavyokiuka sheria.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kulinda haki ya msingi ya uhuru wa kujieleza katika mazingira ya kidijitali, akieleza kuwa hatua za kukabiliana na uhalifu wa mtandao hazipaswi kutumika kama kisingizio cha kukandamiza haki halali za wananchi za kutoa maoni.

Amesema,suluhisho ni kuweka usawa kati ya kulinda uhuru wa kujieleza na kuhakikisha kuwa uhuru huo hautumiki kama kinga ya kufanya uhalifu, kueneza chuki, kutishia watu au kuharibu maisha na mali za wengine.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, matumizi halali na yenye uwajibikaji ya mitandao ya kijamii ni msingi wa kujenga mazingira salama, ya kuaminika na yenye kuheshimiana katika ulimwengu wa kidijitali.

Amesemausalama wa mtandao hauwezi kufanikiwa kwa juhudi za Serikali pekee, bali unahitaji kila mtumiaji kutambua wajibu wake katika kulinda mazingira ya kidijitali.

“Ulinzi wa mazingira ya kidijitali ni jukumu la pamoja. Serikali, kampuni za teknolojia na watumiaji wanapaswa kushirikiana kuhakikisha kuwa mitandao inatumika kwa usalama, uhuru na uwajibikaji,”amesema.

Kileo amehitimisha kwa kuwataka wananchi kuwa makini kabla ya kuchapisha, kusambaza au kushiriki taarifa mtandaoni, akisisitiza kuwa kila mtumiaji anapaswa kutambua kuwa matendo ya kidijitali yanaweza kuwa na madhara makubwa kwa mtu binafsi na jamii kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here