Zanzibar yazindua Kampeni ya Ulinzi wa Mtoto Mtandaoni, Yusuph Kileo apongeza juhudi zinazoendelea za kuhakikisha kila mtoto anakuwa salama nchini

NA DIRAMAKINI

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia
Waziri wa Mawasiliano,Teknolojia ya Habari na Ubunifu imezindua rasmi Kampeni ya Ulinzi wa Mtoto Mtandaoni (Child Online Protection Campaign), hatua inayolenga kuimarisha usalama wa watoto katika matumizi ya teknolojia ya kidijitali huku ikisisitiza ushirikiano wa serikali, sekta binafsi,wataalamu wa usalama wa mtandao na wadau wengine katika kukabiliana na vitisho vinavyowakabili watoto kwenye mazingira ya mtandaoni.
Akizindua kampeni hiyo hivi karibuni,Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu,Mhe. Mudrick Ramadhan Soraga amesema, ulinzi wa watoto katika ulimwengu wa kidijitali ni jukumu la kila mmoja, akieleza kuwa ukuaji wa matumizi ya intaneti na teknolojia za mawasiliano unapaswa kwenda sambamba na mifumo madhubuti ya kuhakikisha watoto wanakuwa salama dhidi ya unyanyasaji, udhalilishaji, ulaghai na aina nyingine za uhalifu wa mtandaoni.

Uzinduzi huo uliwakutanisha viongozi wa serikali, wataalamu wa usalama wa mtandao, wadau wa sekta ya mawasiliano, mashirika ya kiraia pamoja na washirika wa maendeleo kwa lengo la kujadili mikakati ya pamoja ya kuwalinda watoto wanaotumia huduma za kidijitali na kujenga mazingira salama ya matumizi ya teknolojia kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Mtaalamu wa Masuala ya Usalama wa Mtandao na Uchunguzi wa Makosa ya Mtandao, Yusuph Kileo amesema, alipata fursa ya kushiriki uzoefu wa Tanzania Bara kuhusu utekelezaji wa programu za Ulinzi wa Mtoto Mtandaoni, akieleza kuwa nchi imepiga hatua kubwa katika kuimarisha mfumo wa ulinzi wa watoto kwa kuunganisha maboresho ya sheria na utekelezaji wa kampeni za kitaifa.

Amesema,mafanikio hayo yamejengwa kwa kiasi kikubwa kutokana na matokeo ya utafiti wa Disrupting Harm wa mwaka 2022, ambao uliweka bayana changamoto zinazowakabili watoto katika mazingira ya mtandaoni na kusaidia kuandaa mikakati inayozingatia ushahidi na takwimu.

Kwa mujibu wa Kileo, Serikali ya Tanzania imefanya marekebisho ya Sheria ya Makosa ya Mtandao ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia na kuongeza ufanisi katika kukabiliana na uhalifu unaowalenga watoto.

Aidha, imeanzisha Kamati Maalumu ya Kitaifa ya Ushauri kuhusu Ulinzi wa Mtoto Mtandaoni inayoratibu juhudi za taasisi mbalimbali katika kuhakikisha watoto wanalindwa ipasavyo wanapotumia huduma za kidijitali.

Ameongeza kuwa,kupitia kampeni za kitaifa za uelimishaji, zaidi ya wawezeshaji 500 wamepewa mafunzo maalumu yaliyowawezesha kufikisha elimu ya usalama mtandaoni kwa wanafunzi na walimu zaidi ya milioni 1.8 katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.
Hatua hiyo imeongeza uelewa kuhusu matumizi salama ya intaneti, namna ya kutambua vihatarishi vya mtandaoni pamoja na njia za kutoa taarifa pale watoto wanapokumbana na vitendo vya ukatili wa kidijitali.

Kileo amesema,vyombo vya dola kwa kushirikiana na mashirika ya kiraia vinaendelea kutumia Namba ya Kitaifa ya Simu ya Msaada kwa Mtoto 116, ambayo haina malipo, kupokea taarifa za haraka kuhusu unyanyasaji wa watoto mtandaoni, kutoa msaada wa kisaikolojia kwa waathirika pamoja na kuratibu hatua za kisheria dhidi ya wahusika wa vitendo vya unyanyasaji, uonevu na unyonyaji wa watoto kupitia mitandao.

Vilevile, amesisitiza kuwa,mafanikio yaliyopatikana Tanzania Bara yanaonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, taasisi za elimu, wazazi, jamii, sekta binafsi na wataalamu wa usalama wa mtandao katika kujenga mazingira salama ya kidijitali kwa watoto.

Uzinduzi wa Kampeni ya Ulinzi wa Mtoto Mtandaoni Zanzibar unatarajiwa kuimarisha juhudi za kukuza matumizi salama ya teknolojia, kuongeza uelewa wa jamii kuhusu haki na usalama wa watoto katika mazingira ya kidijitali, pamoja na kuimarisha mifumo ya kinga na mwitikio dhidi ya uhalifu wa mtandaoni unaowalenga watoto.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here