NA DIRAMAKINI
SERIKALI ya Afrika Kusini imezindua rasmi mfumo wa Electronic Travel Authorisation (ETA) unaowawezesha wasafiri wanaostahili kutoka China, India, Indonesia na Mexico kukamilisha taratibu za kupata kibali cha kusafiri kwa njia ya kidijitali.
Mfumo huo ulizinduliwa Jumatano, Agosti 12, 2026 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa OR Tambo na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa ambaye amesema, hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuifanya mifumo ya uhamiaji kuwa ya kisasa, yenye ufanisi na salama zaidi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Rais Ramaphosa amesema, mfumo wa ETA utasaidia kurahisisha na kuharakisha taratibu za kusafiri kwenda Afrika Kusini, huku ukiimarisha usalama wa nchi na kuongeza ushindani wake katika uchumi wa dunia.
Mfumo huo unatumia teknolojia mbalimbali za kisasa, ikiwemo uthibitishaji wa alama za kibayometriki, utambuzi wa sura (facial recognition), ujifunzaji wa mashine (machine learning) pamoja na mfumo ulioboreshwa wa kielektroniki wa kudhibiti mienendo ya wasafiri.
Kupitia mfumo huo, waombaji wanaweza kuwasilisha taarifa zao kwa njia ya mtandao, kufanya malipo kidijitali na kupokea kibali chao cha kusafiri kwa njia ya kielektroniki.
Rais Ramaphosa amesema, mageuzi hayo yanalenga kuifanya Afrika Kusini kuwa nchi inayofunguka zaidi kwa fursa, inayowakaribisha wasafiri halali, huku ikiendelea kulinda usalama wa raia wake.
“Mfumo wa Electronic Travel Authorisation unalenga kuifanya Afrika Kusini kuwa wazi zaidi kwa fursa, kuwakaribisha zaidi wasafiri halali, kuwa salama zaidi kwa raia wetu na kuwa na ushindani zaidi katika uchumi wa dunia,” amesema Rais Ramaphosa.
Uzinduzi wa ETA unaashiria hatua nyingine katika mpango wa Afrika Kusini wa kutumia teknolojia za kidijitali kuboresha huduma za uhamiaji na kurahisisha safari za kimataifa, sambamba na kuimarisha uwezo wa mamlaka kuchambua na kuthibitisha taarifa za wasafiri kabla na wakati wa kuingia nchini.
Mfumo huo unatarajiwa pia kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mipaka na kutoa mazingira rafiki zaidi kwa wasafiri wanaokidhi masharti ya kuingia nchini humo.
Tags
Afrika Kusini
Habari
Kimataifa
Kuingia Afrika Kusini
Kuishi Afrika Kusini
Vibali Afrika Kusini
Vigezo Kuingia Afrika Kusini
Visa Afrika Kusini
Wasafiri Afrika Kusini
