Askari watakiwa kuendelea kuimarisha mahusiano na wananchi

RUVUMA-Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Marco G.Chilya amewataka Maafisa, Wakaguzi na Askari kuendelea kujenga na kudumisha mahusiano mazuri na wananchi kwa kutekeleza majukumu yao kwa weledi, haki na uadilifu, huku wakizingatia sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza utendaji wa Jeshi la Polisi.
Wito huo umetolewa wakati akizungumza na Maafisa, Wakaguzi na Askari wa vyeo mbalimbali wa Wilaya ya Namtumbo, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi wilayani humo huku akisisitiza mahusiano mazuri kati ya Jeshi la Polisi na wananchi kwani ndio msingi muhimu katika kujenga imani na ushirikiano wa jamii, ambao unasaidia Jeshi kupata taarifa muhimu za uhalifu na kuchukua hatua stahiki kwa wakati.

Aidha, Kamanda Chilya amewapongeza askari kwa kuendelea kuonesha utayari na kutumia mbinu mbalimbali katika kuhakikisha uhalifu na wahalifu wanadhibitiwa kwa mujibu wa sheria huku akiwasisitiza kuwa juhudi hizo zinapaswa kuendelea kuzingatia misingi ya haki, utu na weledi, ili kuhakikisha watuhumiwa wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Sambamba na hilo, Kamanda Chilya amesisitiza umuhimu wa askari kutoa huduma bora kwa mteja wa ndani na nje wa Jeshi la Polisi huku akiwataka kuwa wasikivu, wenye heshima na kuwajibika wanapohudumia wananchi, huku wakihakikisha kero na malalamiko yao yanapokelewa na kupatiwa ufumbuzi wa haraka kwa mujibu wa sheria.

"Utendaji wenye weledi, uadilifu na uzingatiaji wa sheria ni miongoni mwa mambo yanayoweza kuongeza imani ya wananchi kwa Jeshi la Polisi hivyo askari muendelee kuwa karibu na wananchi, kusikiliza changamoto zao na kushirikiana nao katika kuzuia na kupambana na uhalifu pamoja na kudumisha amani na usalama katika maeneo yao,"amesema Kamanda Chilya.
Sanjari na hilo amewataka askari wa Wilaya ya Namtumbo kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa moyo wa uzalendo na uwajibikaji, wakitambua kuwa usalama wa wananchi na mali zao ni jukumu la msingi la Jeshi la Polisi na kusema kuwa ushirikiano kati ya Polisi na jamii ukiimarishwa zaidi utasaidia kujenga mazingira salama.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here