BoT yaendesha semina kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu muundo na majukumu yake

DODOMA-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendesha semina kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, ikiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Mashimba Ndaki, kuhusu Muundo na Majukumu ya Benki Kuu pamoja na uwekezaji katika dhamana za Serikali.
Semina hiyo imefanyika tarehe 13 Agosti 2026 jijini Dodoma ambapo ujumbe wa Benki Kuu uliongozwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde.

Katika semina hiyo, Wajumbe walielezwa kuwa jukumu la msingi la Benki Kuu ni kuandaa na kutekeleza sera ya fedha inayolenga kudumisha utulivu wa bei na kuhakikisha mfumo wa fedha unaendelea kuwa imara na kuchangia ukuaji endelevu wa uchumi.

Aidha, walielezwa kuwa tangu Januari 2024, Benki Kuu inatumia mfumo wa sera ya fedha unaotumia riba, ambapo Riba ya Benki Kuu (CBR) hutumika kuongoza mwenendo wa viwango vya riba katika masoko ya fedha. Katika robo ya tatu ya mwaka 2026, CBR iliongezwa kutoka asilimia 5.75 hadi 6.25 ili kudhibiti shinikizo la mfumuko wa bei.
Kwa upande wa dhamana za Serikali, Wajumbe walielezwa kuwa Benki Kuu, kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huendesha minada ya dhamana za Serikali kwa lengo la kuwezesha Serikali kupata fedha za kugharamia shughuli na miradi mbalimbali kupitia soko la ndani la fedha.

Dhamana za Serikali zinajumuisha dhamana za muda mfupi (Treasury bills) na hati fungani za Serikali (Treasury bonds).

Dhamana za muda mfupi hutolewa kwa vipindi mbalimbali, ikiwemo siku 35, 91, 182 na 364, huku hati fungani za Serikali zikitolewa kwa vipindi vya miaka 2, 5, 7, 10, 15, 20 na 25.
Semina hiyo imekuwa sehemu ya jitihada za Benki Kuu za kuendelea kuimarisha uelewa wa Wabunge kuhusu majukumu yake, utekelezaji wa sera ya fedha na mwenendo wa masoko ya fedha.

Kupitia semina hiyo, Wajumbe wamepata fursa ya kujadili na kupata ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali yanayohusiana na utulivu wa bei, usimamizi wa mfumo wa fedha na maendeleo ya soko la dhamana za Serikali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here