DAR-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa wito kwa wadau mbalimbali wa sekta ya fedha kuendelea kushirikiana katika jitihada za kuziba pengo la kijinsia katika upatikanaji na utumiaji wa huduma za fedha, ili kuhakikisha wanawake, vijana na wamiliki wa biashara ndogo na za kati wanaweza kunufaika kikamilifu na huduma hizo kwa ajili ya kuboresha maisha na shughuli zao za kiuchumi.

Hayo yameelezwa na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bi. Sauda Msemo, wakati akifungua kikao kazi cha kujadili masuluhisho ya vitendo (practical solutions) kwa ajili ya kuziba pengo la kijinsia katika ujumuishi wa kifedha (Sprints Session on Tanzania: Closing the Gender Gap in Financial Inclusion) kilichowakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya fedha wakiwemo Financial Sector Deepening Tanzania na Alliance for Innovative Regulation, jijini Dar es Salaam.
Katika hotuba yake, amewashukuru Financial Sector Deepening Tanzania (FSDT) na Alliance for Innovative Regulation (AIR) kwa ushirikiano na msaada wa kitaalamu katika kuendeleza mpango wa kuziba pengo la kijinsia katika ujumuishi wa kifedha nchini Tanzania.“Suala la ujumuishi wa kifedha linahitaji ushirikiano wa pamoja wa taasisi za umma, watoa huduma za fedha, benki, kampuni za mawasiliano, Wizara, taasisi za Serikali pamoja na wadau wengine ili kubuni na kutekeleza masuluhisho yatakayowezesha makundi mbalimbali kupata na kutumia huduma za fedha kwa manufaa yao,”amesema.
Ameongeza kuwa, ujumuishi wa kifedha wenye tija unapaswa kupimwa kwa kuangalia namna huduma za fedha zinavyochangia kuboresha ustawi, afya ya kifedha na uwezo wa wananchi kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiuchumi.
Vilevile, alieleza kuwa wanawake na wamiliki wa biashara ndogo na za kati bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali katika kupata huduma rasmi za fedha, hususan mikopo yenye tija.
Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na ukosefu wa dhamana zinazokubalika, changamoto katika mahitaji ya utambuzi wa mteja (Know Your Customer-KYC), historia ndogo ya matumizi ya mikopo pamoja na upungufu wa taarifa muhimu zinazoweza kutumika katika kutathmini uwezo wa mkopaji.
Naibu Gavana huyo amewataka washiriki wa kikao hicho kitakachofanyika tarehe 24 hadi 27 Agosti 2026 kutumia fursa hiyo ya majadiliano kuja na masuluhisho ya vitendo, kukubaliana hatua mahsusi za utekelezaji na kuimarisha ushirikiano utakaowezesha utekelezaji wa mapendekezo yatakayotoa matokeo yanayoonekana.
Kufanikiwa kwa lengo hili kutakuwa na manufaa makubwa katika kuongeza idadi ya watu wanaopata huduma za fedha, ikiwa ni pamoja na kuongeza ushiriki wa wananchi katika shughuli za kiuchumi, uzalishaji, ajira, ustahimilivu wa kaya na ustawi mpana wa kijamii na kiuchumi.
Tags
Benki Kuu ya Tanzania
FSDT
Habari
Huduma Jumuishi za Fedha
Pengo la Kijinsia katika Ujumuishi wa Kifedha
Sekta ya Fedha Tanzania








