Nchimbi ajiuzulu nafasi ya Makamu wa Rais, astaafu siasa na utumishi wa umma Tanzania

NA DIRAMAKINI

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Emmanuel John Nchimbi ametangaza kujiuzulu nafasi hiyo kuanzia Septemba 4, 2026 akisema pia ameamua kustaafu siasa na utumishi wa umma.
Dkt. Nchimbi ametangaza uamuzi huo leo Jumanne, Agosti 25,2026 kupitia taarifa ambayo amesema, ameiwasilisha kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akimjulisha rasmi kuhusu uamuzi wake wa kuachia nafasi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uamuzi wa kujiuzulu umefikiwa kwa kuzingatia Ibara ya 50(2)(c), ikisomwa pamoja na Ibara ya 149(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Dkt.Nchimbi amesema,uamuzi huo pia unatekeleza ahadi aliyompa Rais Samia tarehe 27 Agosti 2025, wakati alipoteuliwa kushika wadhifa huo, kwamba angemsaidia Rais na kulitumikia Taifa kwa uwezo wake wote na kwa uaminifu.

Amesema,wakati huo aliahidi pia kuwa angeachia nafasi hiyo endapo Rais angeona kuna haja ya kuwa na Makamu mwingine wa Rais.

“Nimejiridhisha pasipo shaka kuwa Mhe. Rais anatamani mabadiliko, hivyo nimeamua kutimiza ahadi yangu,”amesema Dkt. Nchimbi katika taarifa yake.

Uamuzi huo unamfanya Dkt. Nchimbi kuhitimisha safari yake katika nafasi ya pili kwa ukubwa katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya kuhudumu katika wadhifa huo kwa kipindi kisichofika mwaka mmoja.

Katika taarifa yake, Dkt. Nchimbi amemshukuru Rais Samia kwa imani aliyompa na nafasi ya kumtumikia katika Serikali, pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kumuamini na kumpa fursa ya kushiriki katika uongozi wa Taifa.

Aidha, amewashukuru Watanzania kwa ushirikiano na sapoti waliompa katika kipindi chote cha utumishi wake wa umma.

Pamoja na kutangaza kustaafu siasa na utumishi wa umma, Dkt. Nchimbi amesema, ataendelea kuwa raia mwema wa Tanzania na kushiriki katika maisha ya Taifa kwa nafasi ya uraia.

Dkt.Nchimbi aliteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 27 Agosti 2025, kabla ya kuapishwa rasmi kushika wadhifa huo Novemba 3, 2025.

Kwa mujibu wa Katiba, Makamu wa Rais ni msaidizi mkuu wa Rais katika mambo yote ya Jamhuri ya Muungano na ana majukumu mbalimbali yanayohusiana na utekelezaji wa shughuli za Muungano pamoja na majukumu mengine anayokabidhiwa na Rais.

Nini hutokea Makamu wa Rais anapojiuzulu?

Kujiuzulu kwa Makamu wa Rais si ukomo wa Serikali katika hali ya kutokuwa na mtu wa kushika nafasi hiyo kwa muda usiojulikana.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka utaratibu maalumu wa kujaza nafasi hiyo inapokuwa wazi kutokana na kujiuzulu, kifo au mazingira mengine yanayotajwa katika Katiba.

Ibara ya 50(2)(c) inatambua kujiuzulu kama moja ya sababu zinazoweza kumaliza muda wa Makamu wa Rais katika madaraka.

Baada ya nafasi hiyo kuwa wazi, Ibara ya 50(4) inaelekeza kuwa Rais atateua mtu mwingine kuwa Makamu wa Rais mapema iwezekanavyo na, kwa vyovyote vile, ndani ya siku zisizozidi 14 tangu Makamu wa Rais aliye madarakani kuacha nafasi hiyo.

Uteuzi huo hauwi wa mwisho moja kwa moja,kwani mtu anayeteuliwa na Rais anatakiwa kuthibitishwa na Bunge kwa kura ya Wabunge walio wengi.

Aidha,baada ya uteuzi wake kuthibitishwa na Bunge, Ibara ya 48(2) inaeleza kuwa Makamu wa Rais huyo ataapa na kuanza rasmi kutekeleza majukumu ya wadhifa huo.

Kwa hiyo, iwapo Dkt. Nchimbi ataacha rasmi nafasi hiyo Septemba 4, 2026 kama alivyotangaza, hatua inayofuata kikatiba itakuwa Rais Samia kumteua mtu mwingine ndani ya muda uliowekwa na Katiba, kisha jina hilo kuwasilishwa Bungeni kwa ajili ya kuthibitishwa.

Bunge lina nafasi gani?

Katika mchakato huo, Bunge lina jukumu la kuthibitisha uteuzi wa mtu atakayependekezwa na Rais. Katiba inaweka hitaji la kura ya wengi ya Wabunge kwa ajili ya kuthibitisha uteuzi huo.

Hivyo, mchakato wa kumpata Makamu mpya wa Rais unahusisha hatua kuu tatu: kujiuzulu au kuondoka kwa Makamu wa Rais aliyepo madarakani, uteuzi wa mrithi na Rais, na kuthibitishwa kwa uteuzi huo na Bunge.

Baada ya kuthibitishwa, Makamu wa Rais mteule ataapa mbele ya mamlaka husika kabla ya kuanza rasmi kutekeleza majukumu yake.

Kwa msingi huo, kujiuzulu kwa Dkt. Nchimbi hakumaanishi kuibuka kwa uchaguzi mpya wa Makamu wa Rais. Badala yake, Katiba imeweka utaratibu wa moja kwa moja unaompa Rais mamlaka ya kuteua mtu mwingine, huku Bunge likiwa na jukumu la kuthibitisha uteuzi huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here