Chungu na tamu za miaka 27 ya utawala wa Mfalme Mohammed VI nchini Morocco

NA DIRAMAKINI

MFALME wa Morocco, Mohammed VI ameendelea kupata pongezi kutoka kwa viongozi mbalimbali duniani kutokana na maendeleo ya kiuchumi na kuongezeka kwa ushawishi wa nchi hiyo barani Afrika na kimataifa, wakati akiadhimisha miaka 27 tangu alipoingia madarakani.
Maadhimisho hayo yamefanyika wakati Morocco ikiendelea kujijenga kama moja ya mataifa yenye uchumi unaokua kwa kasi barani Afrika, huku nchi hiyo ikitajwa kuwa imeipita Afrika Kusini katika uzalishaji wa viwandani.

Hata hivyo, sherehe hizo zimekuja sambamba na changamoto za kijamii na kikanda, ikiwemo ongezeko la wahamiaji wanaojaribu kuingia katika eneo la Ceuta, linalodhibitiwa na Hispania kwenye pwani ya Afrika Kaskazini.

Hali hiyo imeongeza shinikizo kwa Madrid kutoka kwa mataifa mengine ya Ulaya na kuibua mjadala kuhusu changamoto za kijamii zinazoendelea kuwepo licha ya mafanikio ya Morocco katika uchumi.

Takwimu za Umoja wa Ulaya zinaonesha kuwa, takribani raia 275,000 wa Morocco walibainika kuwa katika hali isiyo halali ya ukaazi katika nchi wanachama wa umoja huo kati ya mwaka 2021 na 2025, wakiwemo waliokiuka muda wa visa pamoja na watu ambao huenda walihesabiwa zaidi ya mara moja.

Licha ya changamoto hizo, Mfalme Mohammed VI ameadhimisha Siku ya Kiti cha Enzi katika Ikulu ya Kifalme mjini Tetouan, ambapo amepokea jumbe za pongezi kutoka kwa wafalme, wakuu wa nchi na viongozi mbalimbali duniani.

Miongoni mwa viongozi waliomtumia pongezi ni Mfalme Charles III wa Uingereza, Mfalme Willem-Alexander wa Uholanzi, Mfalme Philippe wa Ubelgiji, Mfalme Carl XVI Gustaf wa Sweden na Mfalme Abdullah II wa Jordan.

Viongozi wengine waliotoa pongezi ni Sultani Haitham bin Tarik wa Oman, Mfalme Hamad bin Isa Al Khalifa wa Bahrain na Mwana wa Mfalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman.

Kutoka nje ya falme, jumbe za pongezi zilitumwa pia na Rais wa China Xi Jinping, Rais wa Urusi Vladimir Putin, Rais wa Misri Abdel Fattah El-Sissi na Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye.

Jumbe hizo zimeendelea kuimarisha taswira ya Mohammed VI kama kiongozi anayehusishwa kwa karibu na mabadiliko ya kiuchumi ya Morocco pamoja na kuongezeka kwa ushawishi wa kidiplomasia wa nchi hiyo.

Kutoka uchumi tegemezi hadi nguvu ya viwanda

Mohammed VI alirithi ufalme huo mwaka 1999, baada ya kifo cha baba yake, Mfalme Hassan II, wakati Morocco ikiwa imepitia miaka ya ukuaji wa uchumi uliokuwa ukisuasua.

Wakati huo, uchumi wa nchi hiyo ulitegemea kwa kiasi kikubwa kilimo, utalii, mauzo ya madini ya fosfeti na fedha zilizotumwa na raia wa Morocco wanaoishi nje ya nchi.

Uwezo wa viwanda ulikuwa bado mdogo, huku ukosefu wa ajira na umaskini katika maeneo ya vijijini ukiendelea kuwa changamoto kwa sehemu kubwa ya wananchi.

Katika kipindi cha utawala wake, Morocco imewekeza kwa kiwango kikubwa katika bandari, barabara, reli za mwendo kasi, nishati jadidifu na maeneo maalumu ya viwanda.

Miongoni mwa miradi iliyobeba mabadiliko hayo ni Bandari ya Tangier Med, ambayo imekua na kuwa miongoni mwa bandari muhimu barani Afrika, ikiifanya Morocco kuwa lango la biashara linalounganisha Afrika na Ulaya pamoja na masoko mengine ya kimataifa.

Morocco yageuka kitovu cha magari na anga

Morocco pia imejijengea nafasi kama kitovu muhimu cha uzalishaji wa magari na bidhaa za sekta ya anga, baada ya kuvutia kampuni mbalimbali za kimataifa kuanzisha viwanda na mitandao ya wasambazaji.

Mafanikio hayo yamechangiwa na miundombinu, mikataba ya biashara na nchi nyingine pamoja na ukaribu wa kijiografia na soko la Ulaya.

Kutokana na mabadiliko hayo, pato la taifa kwa kila mwananchi nchini Morocco limekaribia kuongezeka mara mbili tangu mwishoni mwa miaka ya 1990.

Uchumi wa Morocco ulikua kwa takribani asilimia 4.8 mwaka 2025, huku ukitarajiwa kukua kwa asilimia 4.4 mwaka 2026, ukisaidiwa na sekta ya kilimo pamoja na uwekezaji katika miundombinu.

Uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje ya nchi pia uliongezeka kwa kiasi kikubwa, ukifikia takribani dola bilioni 3.34 mwaka 2025, ukichochewa kwa sehemu na uwekezaji katika magari yanayotumia umeme, utengenezaji wa betri na miradi ya nishati safi.

Pamoja na mafanikio ya kiuchumi, Morocco imeendelea kuimarisha uwezo wake wa kijeshi wakati ushindani wa kimkakati ukiongezeka katika Afrika Kaskazini.

Nchi hiyo ilisaini mpango wa miaka 10 wa ushirikiano wa ulinzi na Marekani, unaohusu kipindi cha 2026 hadi 2036.

Morocco pia imepata idhini ya uwezekano wa kununua makombora ya Stinger yenye thamani ya takribani dola milioni 825, pamoja na makombora ya angani kwa angani yenye thamani ya zaidi ya dola milioni 88.

Aidha, Morocco imeagiza helikopta 24 aina ya AH-64E Apache, huku ikihusishwa na uwezekano wa kununua ndege za kivita aina ya F-35.

Iwapo mpango huo wa F-35 utakamilika, Morocco inaweza kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kutumia ndege hizo za kivita zenye teknolojia ya kujificha kwenye rada.

Kwa kuongezeka kwa matumizi ya ulinzi mwaka 2025 na uwekezaji katika vifaa vya kisasa vya kijeshi, Morocco imeendelea kujiimarisha miongoni mwa mataifa yenye nguvu kubwa za kijeshi katika Afrika Kaskazini.

Changamoto bado zipo

Pamoja na mafanikio hayo, Morocco bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi, ikiwemo masuala ya ajira, tofauti za maendeleo kati ya maeneo ya mijini na vijijini pamoja na shinikizo la uhamiaji.

Hali hiyo inaonesha kwamba ukuaji wa uchumi pekee hauondoi changamoto zote zinazokabili jamii.

Hata hivyo, katika kipindi cha miaka 27 ya utawala wa Mohammed VI, Morocco imepiga hatua kubwa katika kubadilisha muundo wa uchumi wake kutoka kutegemea zaidi kilimo, utalii na fosfeti hadi kujenga msingi mpana wa viwanda, usafirishaji, teknolojia, magari, anga na nishati safi.

Kwa mtazamo mpana, safari ya Morocco chini ya Mohammed VI inatoa mfano wa namna uwekezaji katika miundombinu, viwanda, nishati na mahusiano ya kimataifa unavyoweza kutumika kuibadilisha nafasi ya taifa katika uchumi wa bara na dunia.

Hata hivyo, changamoto ya msingi kwa Morocco katika hatua inayofuata itakuwa kuhakikisha mafanikio hayo ya kiuchumi yanatafsirika moja kwa moja katika kuboresha maisha ya wananchi wote, kupunguza tofauti za kijamii na kiuchumi na kutoa fursa zaidi kwa vijana.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here