NA GODFREY NNKO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50 pamoja na Jukwaa la Miundombinu Afrika, utakaofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Agosti 5 hadi 6, 2026.
Mkutano huo utafanyika katika ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam na unatarajiwa kuwakutanisha takribani washiriki 1,200 wakiwemo viongozi wa Serikali, taasisi za fedha za kimataifa.
Aidha, washiriki wengine ni wanahisa wa Africa50, wawekezaji, viongozi wa sekta binafsi na wadau wa maendeleo kutoka Afrika na sehemu mbalimbali duniani.
Waziri wa Fedha,Mheshimiwa Balozi Khamis Mussa Omar ameyasema hayo leo Agosti 3,2026 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini.
Amesema, Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo ni heshima kubwa na ishara ya kuongezeka kwa imani ya jumuiya ya kimataifa kwa nchi katika masuala ya biashara, uwekezaji na maendeleo ya miundombinu.
Balozi Omar amesema,mkutano huo utakuwa jukwaa muhimu la kujadili namna ya kuongeza kasi ya uwekezaji katika miradi ya kimkakati ya miundombinu barani Afrika kwa kuwakutanisha Serikali, sekta binafsi, taasisi za fedha na wawekezaji.
Africa50 yatimiza miaka 10
Pia,Waziri wa Fedha amesema kuwa, mkutano huo unafanyika wakati Africa50 ikitimiza miaka 10 tangu ilipoanza rasmi shughuli zake mwaka 2016.
Mkutano wa mwaka huu umebeba kaulimbiu “A Decade of Economic Impact: From Ambition to Delivery”, inayosisitiza safari ya miaka 10 ya Africa50 kutoka kwenye azma na mipango hadi utekelezaji na matokeo ya kiuchumi.
Taasisi hiyo ilianzishwa mwaka 2013 kwa ushirikiano wa Serikali za Afrika na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), kufuatia uamuzi wa Wakuu wa Nchi za Afrika wa kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya miundombinu kupitia Programme for Infrastructure Development in Africa (PIDA), ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Umoja wa Afrika ya Agenda 2063.
Amesema, Africa50 yenye makao makuu Casablanca nchini Morocco, hushirikiana na Serikali za Afrika katika kuandaa na kuendeleza miradi ya miundombinu hadi kufikia hatua ya kuvutia uwekezaji, pamoja na kuhamasisha mitaji kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo kupitia ubia kati ya Serikali na sekta binafsi (PPP).
Sekta zinazolengwa na taasisi hiyo ni pamoja na nishati, uchukuzi, elimu, afya, TEHAMA na huduma za kifedha, ikiwemo teknolojia za kifedha.
Tanzania mwanahisa wa Africa50
Waziri wa Fedha amesema,Tanzania ilijiunga rasmi na Africa50 tarehe 14 Februari 2023 kama mwanahisa wa kundi la “A”, linalojumuisha nchi huru za Afrika.
Amesema,uanachama huo umeongeza fursa kwa Tanzania kushiriki katika maandalizi, uendelezaji na ufadhili wa miradi mikubwa ya kimkakati ya miundombinu.
Tangu kujiunga kwake, Tanzania imeanza kunufaika na ushirikiano huo kupitia hatua za maandalizi na uendelezaji wa miradi mbalimbali.
Miongoni mwa miradi ambayo Africa50 imeanza kushirikiana na Serikali kuandaa na kuitathmini ni maendeleo ya Bandari ya Mangapwani Zanzibar, Mradi wa Mini Liquefied Natural Gas (Mini LNG).
Vilevile, miradi ya miundombinu ya usafirishaji wa umeme, pamoja na miradi ya afya, hususan upanuzi wa huduma za usafishaji wa figo (dialysis) kupitia ubia kati ya sekta ya umma na binafsi.
Fursa kwa Tanzania
Kwa Tanzania, Waziri wa Fedha amesema kuwa, mkutano huo unatarajiwa kuwa zaidi ya mkusanyiko wa viongozi na wawekezaji,kwani pia ni jukwaa la kutangaza fursa za uwekezaji na miradi ya kimkakati ya nchi kwa wawekezaji wa ndani na nje.
Mkutano huo utashirikisha taasisi mbalimbali za umma na sekta binafsi nchini, zikiwemo benki za biashara na maendeleo, taasisi za hifadhi ya jamii, taasisi za uwekezaji na masoko ya mitaji pamoja na wadau wanaohusika na sekta za nishati, ujenzi, uchukuzi, reli, bandari, usafiri wa anga, maji, afya, madini, mafuta na gesi na TEHAMA.
Balozi Omar amesema, uwepo wa wadau hao unalenga kuongeza nafasi za kujenga ushirikiano, kubadilishana uzoefu na kutengeneza fursa za mitaji kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mambo makuu yatakayojadiliwa
Katika siku mbili za mkutano, shughuli kuu zitakazofanyika ni pamoja na Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50 (GSM), Jukwaa la Miundombinu Afrika (Infra for Africa Forum) na hafla za kusaini makubaliano mbalimbali yanayohusu maandalizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya miundombinu.
Mkutano huo unatarajiwa kutoa nafasi ya kujadili changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa miradi mikubwa barani Afrika, ikiwemo upatikanaji wa fedha, maandalizi ya miradi inayoweza kuvutia wawekezaji, ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi na matumizi ya ubunifu katika kuongeza ufanisi wa miundombinu.
Mchango kwa uchumi wa Tanzania
Kwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo, Waziri wa Fedha amesema,Tanzania inatarajiwa kupata fursa ya kujiimarisha kama kitovu cha biashara, uwekezaji na maendeleo ya miundombinu katika Afrika Mashariki.
Aidha, mkutano huo unaweza kuchochea shughuli za biashara, uwekezaji, utalii wa mikutano (MICE), ubia kati ya Serikali na sekta binafsi pamoja na kuimarisha mahusiano ya kiuchumi kati ya Tanzania na mataifa mbalimbali.
Kwa upande mwingine, uwepo wa wawekezaji na viongozi wa taasisi za fedha katika mkutano huo unatoa fursa kwa Tanzania kuendelea kuwasilisha miradi yake ya kimkakati na kutafuta washirika wa kifedha na kiteknolojia kwa ajili ya utekelezaji wake.
Serikali imesema maandalizi ya mkutano huo yanaendelea vizuri kwa kushirikiana na Africa50 pamoja na taasisi mbalimbali za Serikali, huku wananchi wakihimizwa kutoa ushirikiano na kuwakaribisha wageni watakaofika nchini kwa ajili ya mkutano huo.
Kwa ujumla, Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50 na Jukwaa la Miundombinu Afrika kunatarajiwa kuongeza mwonekano wa nchi katika ramani ya uwekezaji barani Afrika, huku ukitoa nafasi ya kuvutia mitaji, teknolojia na ubia unaoweza kuchochea utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kwa manufaa ya uchumi wa Taifa.
Tags
Africa50
Balozi Khamis Mussa Omary
Dr Samia Suluhu Hassan
Habari
Kimataifa
Wizara ya Fedha Tanzania
