GST yaendelea kuimarisha uwezo wake wa tafiti

DODOMA-Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imeendelea kuimarisha uwezo wake wa kitaalamu kwa kuwekeza katika mafunzo na ushirikiano na taasisi mbalimbali za kitaifa na kimataifa, hatua iliyowezesha watumishi wake kupata ujuzi na mbinu za kisasa katika kufanya tafiti za jiosayansi na uchunguzi wa sampuli maabara.
Akizungumza alipotembelea banda la GST katika Maonesho ya Wakulima ya Nane Nane yanayoendelea jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Utawala na Uendeshaji wa GST, Bi. Neema Morice Mhagama, amesema ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia taasisi imekuwa ikijengea watumishi wake uwezo kupitia mafunzo na ushirikiano na taasisi nyingine za kitafiti za ndani na nje ya nchi.

Mashirikiano hayo yameendelea kuimarisha uwezo wa wataalamu wa GST kwa kubadilishana uzoefu na teknolojia.

Bi Mhagama amesema taasisi hiyo imekuwa na mashirikiano na taasisi mbalimbali ikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Dodoma na taasisi za nje ni pamoja na Taasisi ya Jiolojia ya Uingereza, Finland, Korea Kusini, na China.
Amesema,kupitia mafunzo, kubadilishana uzoefu na programu mbalimbali za ushirikiano wa kitaalamu, watumishi wa GST wamepata maarifa na teknolojia mpya yanayochochea ubunifu, ufanisi katika tafiti za jiosayansi na kuboresha huduma zinazotolewa kwa wachimbaji, wawekezaji na wadau wengine wa Sekta ya Madini.

Aidha, ili kuwezesha uchimbaji wenye tija Mhagama amewahimiza wadau wa Sekta ya Madini kuwatumia wataalamu wa GST katika shughuli zao za uchimbaji kwa kupata taarifa za uhakika wa miamba na namna bora ya uchimbaji na uchukuaji wa sampuli za miamba.
Vilevile, Bi. Mhagama amewaalika wadau waliopo Dodoma na maeneo mengine kutembelea banda la GST katika Maonesho hayo ya Nane Nane yanayoendelea jijini Dodoma ili kujifunza masuala mbalimbali ya madini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here