NA GODFREY NNKO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amesisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuimarisha uwekezaji katika miundombinu inayoweza kuhimili mabadiliko ya kiuchumi, kisiasa na kimazingira, huku akitoa wito wa kuunganisha mataifa ya bara hilo ili kukuza biashara, uwekezaji na uongezaji thamani wa rasilimali.
Ameyasema hayo leo Agosti 5,2026 jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Taasisi ya Africa50 pamoja na Jukwaa la Miundombinu Afrika (Infra for Africa Forum).
Tanzania ni mwenyeji wa mikutano hiyo inayofanyika Agosti 5 na 6, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC).
Mikutano hiyo imefanyika katika kipindi ambacho Africa50 inatimiza miaka 10 tangu kuanzishwa kwake, ikiwa ni jukwaa linalolenga kuunganisha mitaji, miradi na wataalamu kwa ajili ya kuharakisha maendeleo ya miundombinu barani Afrika.
Katika hotuba yake, Rais Dkt.Samia amesema, Tanzania inaendelea kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi katika kuimarisha miundombinu muhimu ikiwemo barabara, reli, bandari na viwanja vya ndege, akibainisha kuwa uwekezaji huo una mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Taifa.
Amesema,miundombinu bora inawezesha kupunguza gharama za usafirishaji, kukuza biashara, kuvutia uwekezaji na kuongeza ajira, huku ikiimarisha nafasi ya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa Rais Dkt.Samia, mabadiliko yanayoendelea kutokea duniani katika nyanja za uchumi, siasa na mazingira yanaifanya Afrika kuwa na umuhimu wa kujenga miundombinu inayoweza kukabiliana na changamoto hizo na wakati huo huo kuunganisha nchi za bara hilo.
Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amesema, hatua hiyo itasaidia Afrika kuongeza biashara baina ya nchi, kuvutia mitaji, kuchochea uwekezaji na kuhakikisha rasilimali zinazozalishwa barani humo zinaongezewa thamani kabla ya kuuzwa katika masoko ya nje.
TANZANIA YAENDELEA KUIPA KIPAUMBELE AFRICA50
Kwa upande wake Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Balozi Khamis Mussa Omar amesema, Tanzania itaendelea kushirikiana na Africa50 kutokana na mchango wa taasisi hiyo katika kuandaa miradi, kuhamasisha uwekezaji na kufadhili miradi ya miundombinu kupitia ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi.
Balozi Omar amesema,Africa50 imejijengea heshima katika kipindi cha miaka 10 kwa kuwa miongoni mwa taasisi zinazoongoza Afrika katika kuandaa miradi ya miundombinu, kukusanya mitaji na kujenga ushirikiano wa kimkakati.
Amesema,mafanikio ya taasisi hiyo katika muongo mmoja uliopita yanaonesha kuwa taasisi zinazoongozwa na Waafrika zinaweza kuandaa na kutekeleza miradi mikubwa yenye uwezo wa kubadilisha uchumi wa bara hilo.
Ameeleza kuwa kaulimbiu ya mkutano huo, “Muongo Mmoja wa Athari za Kiuchumi: Kutoka Kwenye Nia Mpaka Kwenye Utekelezaji,” inasisitiza umuhimu wa kubadilisha maono ya maendeleo kuwa miradi halisi yenye tija kwa wananchi.
"Maendeleo endelevu hayapatikani tu kwa kuwa na maono, bali kupitia ushirikiano thabiti kati ya Serikali, taasisi za kifedha za maendeleo, wawekezaji na sekta binafsi ili kubadilisha mawazo kuwa miradi yenye tija na fursa za kiuchumi za kudumu kwa watu wetu,” amesema.
MIUNDOMBINU NGUZO YA UCHUMI WA TANZANIA
Balozi Omar amesema, Tanzania inaendelea kuifanya miundombinu kuwa sehemu muhimu ya ajenda ya Taifa ya kukuza viwanda na ajira, akitaja mitandao ya kisasa ya usafiri, nishati, miundombinu ya kidijitali na vituo vya usafirishaji kuwa miongoni mwa maeneo yanayopewa kipaumbele.
Amesema,Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia inaendelea kutekeleza ajenda ya mabadiliko ya kiuchumi inayotegemea uwekezaji wa kimkakati katika miundombinu, mtengamano wa kikanda, ushirikishwaji wa sekta binafsi na uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji.
Kwa sababu hiyo, amesema Tanzania itaendelea kuwa mwanahisa wa Africa50 kwa kuwa inaamini katika mfumo wa taasisi hiyo wa kuunganisha rasilimali, mitaji na utaalamu kwa ajili ya kuchochea maendeleo endelevu barani Afrika.FURSA ZA UFADHILI WA MIRADI
Balozi Omar amesema, mkutano huo wa siku mbili unatoa fursa kwa Serikali, wawekezaji na taasisi za fedha kujadili mbinu mbadala za ufadhili wa miradi ya miundombinu na kujenga ushirikiano wa kimkakati.
Amesema majadiliano hayo ni muhimu katika kubaini suluhisho la mahitaji ya kifedha yanayokabili utekelezaji wa miradi ya miundombinu barani Afrika, ambayo ikikamilika inaweza kufungua fursa mpya za kiuchumi na kuongeza kasi ya maendeleo.
Aidha, ameishukuru Africa50 kwa kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo, akisema hatua hiyo ni ishara ya imani kwa Tanzania na uwezo wa Afrika Mashariki katika kukuza maendeleo, kuimarisha uunganishaji wa kikanda na kufanikisha ustawi wa pamoja wa bara.
AFRICA50 YATAJA MAFANIKIO YA MIAKA 10
Nate Afisa Mtendaji Mkuu wa Africa50, Alain Ebobisse, amesema taasisi hiyo inapoingia katika muongo wa pili tangu kuanzishwa kwake, inajivunia mchango wake katika kuendeleza miundombinu ya Afrika na kuweka msingi wa kuongeza uwekezaji katika sekta mbalimbali.
Amesema,miundombinu imekuwa msingi wa kuharakisha uwekezaji katika nishati, usafiri, miundombinu ya kidijitali, usalama wa miundombinu na mifumo ya fedha, kwa lengo la kuifanya Afrika kuwa kitovu cha uwekezaji wenye ushindani duniani.
Ebobisse amesema, katika kipindi cha miaka 10, Africa50 imeshiriki katika miradi 26 yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni moja katika nchi mbalimbali za Afrika.
Amesema, kupitia Africa50 Infrastructure Acceleration Fund, taasisi hiyo imefanikiwa kukusanya zaidi ya dola milioni 300 kutoka kwa wawekezaji 26, ambapo 23 kati yao ni Waafrika.
Kwa mujibu wa Ebobisse, ushiriki huo unaonesha kuwa Afrika ina uwezo wa kutumia mtaji wake wa ndani kufadhili na kuchochea maendeleo ya bara, badala ya kutegemea kwa kiwango kikubwa rasilimali kutoka nje.
AFRICA50 YALENGA DOLA BILIONI 5
Akizungumzia mipango ya muongo ujao, Ebobisse amesema, Africa50 inalenga kuongeza mtaji unaosimamiwa hadi kufikia dola za Marekani bilioni tano, hatua inayotarajiwa kuchochea zaidi ya dola bilioni 30 za uwekezaji kutoka sekta binafsi.
Amesema, uwekezaji huo unatarajiwa kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika sekta za nishati, uchumi wa kijani, usafiri na miundombinu ya kidijitali.
Amesema, mkakati huo unalenga kuongeza uwezo wa Afrika kutumia rasilimali zake za ndani katika kujenga miundombinu na kuchochea ukuaji wa uchumi kwa muda mrefu.
GESI ASILIA ITUMIKE KUCHOCHEA VIWANDA
Ebobisse pia amesisitiza umuhimu wa Afrika kutumia rasilimali zake za gesi asilia kama kichocheo cha uwekezaji na maendeleo ya viwanda.
Amesema, gesi asilia inaweza kutumika kuongeza upatikanaji wa nishati inayohitajika kuendesha viwanda, kuongeza uzalishaji wa kilimo, kuchochea uongezaji thamani wa madini na kuboresha huduma za afya pamoja na usafiri.
Kwa mujibu wake, matumizi yenye tija ya rasilimali hizo ni sehemu muhimu ya kujenga msingi wa mapinduzi ya viwanda na ukuaji endelevu wa uchumi wa Afrika.
Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50 na Jukwaa la Miundombinu Afrika umewakutanisha viongozi wa Serikali, wawekezaji, taasisi za fedha na wadau mbalimbali kutoka Afrika na maeneo mengine kwa lengo la kujadili namna ya kuongeza uwekezaji katika miundombinu na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati.















